Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi. Angela Anathory akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo mpya wa kuomba huduma za RITA utakaoanza kutumika kwaajili ya kuwasaidia wananchi kupata huduma mbalimbali wanazozitoa kwa njia ya Kidijitali.
Meneja wa Usajili wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Patricia Mpuya akitoa mada kwa Wahariri iliyohusu Huduma mbalimbali zitolewazo na Taasisi hiyo.
Mkurugenzi wa TEHAMA wa (RITA) Bi. Rhobi Otaigo akizungumza kuelezea mfumo mpya wa Kidijitali utakaoanza kutumika kutoa huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile akizungumza alipokuwa akitoa neno la utangulizi akimkaribisha Mtendaji Mkuu wa RITA kutoa hotuba yake. (katikati aliyekaa), ni Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi. Angela Anathory na, (kulia), ni Makamu Mwenyekiti wa TEF Bakari Machumu.Â
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya (TEF) Neville Meena akizungumza alipokuwa akitoa mada katika mkutano huo.
Maofisa wa RITA wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Tendaji ya (TEF) Neville Meena alipokuwa akiwasilisha mada katika Mkutano huo.Â
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
(Picha Mbalimbali za Wahariri katika mkutano huo)
MOROGORO.
ZAIDI ya watoto milioni nane walio na umri chini ya miaka mitano hapa nchini wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Takwimu hizo zimetangazwa leo April 1,2023 na Mtendaji Mkuu wa RITA, Bi.Angela Anathory wakati wa Mkutano Mkuu wa 12 wa Kitaaluma wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) uliofanyika Mkoani Morogoro.
Katika mkutano huo RITA wamepata fursa ya kuelezea maboresho waliyofanya katika utoaji wa huduma zao ambapo wameanzisha mfumo mpya utakaosaidia wananchi kupata huduma kwa njia ya mtandao.
“RITA tumeanzisha mfumo mpya wa kuomba huduma Kidijitali unaojulikana kama (eRITA), mfumo huu utawafikia watu wengi kusajili na kupatiwa vyeti wakiwemo watoto”
“Mfumo huo utalenga kutoa vyeti vya Vizazi, vifo, watoto, Ndoa na Udhamini” amesema angela.
Chini ya mfumo huo Bi. Angela amesema kuwa utamwezesha mtu kujisajili mahali popote alipo na kisha atafika tu katika Ofisi za RITA kwa ajili ya kupatiwa vyeti husika.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu huyo, umbali na muda vilikuwa ni vitu vinavyokwamisha upatikanaji wa vyeti kwa wananchi jinsi ya kuvipata, hivyo uwepo wa mfumo mpya wa eRITA utasaidia zaidi kusajili wananchi.
Katika hatua nyingine Bi. Angela amezungumzia hali ya wananchi katika kuandika WOSIA ambapo amesema kuwa hadi sasa wananchi 193 ndio walioandika WOSIA na kuufikisha katika Ofisi za RITA kuhifadhiwa.
Kutokana na idadi hiyo kuwa ndogo, RITA imetoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia na wasiogope kwani sio uchuro kama inavyodaiwa.
MWISHO.