Sehemu ya vyumba vya madarasa ya shule ya Sekondari Kungu wilayani Tunduru kama yanavyoonekana,kujengwa kwa shule hiyo mpya ni mpango wa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu na kusogeza elimu kwa watoto ili kuwaondolea changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda shule nyingine kufuata masomo.
Jengo la Utawala katika shule mpya ya Sekondari Kungu wilayani Tunduru ambayo imeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu.
Kaimu Afisa elimu Sekondari wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mwalimu Stephen Makina katikati,Diwani wa kata ya Nakayaya Daud Amlima wa tatu kushoto Kaka Mkuu wa shule hiyo Tariq Mnupate wa pili kushoto na Dada Mkuu Iqra Hamis na Makamu mkuu wa shule Yasin Songwe wa kwanza kulia, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa shule hiyo
Na: Muhidin Amri, Tunduru
SERIKALI kupitia mradi wa kuboresha elimu ya sekondari nchini(SEQUIP) ,imeipatia Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,jumla ya Sh.bilioni 1,410,000,000 kwa ajili kujenga shule mpya tatu za Sekondari ikiwa ni mkakati wake wa kuboresha sekta ya elimu na kupunguza makali ya wanafunzi kwenda umbali mrefu kufuata masomo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Chiza Marando amezitaja shule hizo mpya ni Majimaji iliyopangiwa kupokea wanafunzi 170,Kungu wanafunzi 220 na Mpakate 214 na zimeanza kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza wa muhula wa masomo 2023.
Alisema katika shule hizo kuna majengo ya maabara, utawala, vyoo, mfumo wa maji,maktaba na jengo la TEHAMA ambayo yatawezesha wanafunzi kuwa na wigo mpana wa kujisomea na walimu kupata mazingira bora ya kufundishia.
Aidha alisema,Halmashauri imepokea Sh.milioni 200,000,000 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu zilizotumika kujenga madarasa 10 kwenye shule sita za sekondari katika za Matemanga, Semeni, Ligoma, Kidodo
“Na sisi kama Halmashauri ya wilaya kupitia mapato yetu ya ndani tumeongeza Sh.milioni 301,069,168 kwa ajili ya kujenga na kuboresha miundombinu ya shule ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na sehemu nzuri ya kujifunza na walimu kufundishia” alisema Marando.
Marando amesisitiza,watahakikisha kila mwanafunzi aliyechaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari anapokelewa shuleni kwa kuwa tayari serikali imeondoa ada elimu ya msingi hadi kidato cha sita ili watoto wengi wa Kitanzania waweze kupata elimu.
Amewataka wazazi na walezi wenye watoto wanaopaswa kuingia kidato cha kwanza mwaka huu kuwapeleka shule bila kujali hali walizo nazo kwa kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kila mtoto anapata elimu.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Kungu Rehema Ngunguni,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kujenga shule mpya ambayo imemaliza kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kusoma katika shule za kata nyingine.
Rehema ameshukuru uamuzi wa serikali ya kutoa nafasi ya wanafunzi wasiokuwa na mahitaji ikiwamo sare kuendelea na masomo yao na kueleza kuwa,hatua hiyo itasaidia watoto wengi wanaotoka kwenye familia maskini kupata elimu.
Makamu mkuu wa shule hiyo Yasin Songwe alisema, wamepangiwa kupokea wanafunzi 220 na hadi sasa wanafunzi 143 kati 79 wavulana na 65 wa kike ambapo mwitio ni mkubwa sana.
Alisema,awali wanafunzi wanatoka katika kata ya Nakayaya walilazimika kwenda kusoma shule ya Sekondari Mgomba au Mataka umbali wa km 8 hivyo kwa kiasi kikubwa kuwaathiri sana kimasomo.
Diwani wa kata ya Nakayaya Daud Amlima alisema,shule hiyo mpya itahamasisha watoto wengi wanaomaliza darasa la saba kupenda na kuendelea na masomo yao ya Sekondari na watahakikisha wanakuwa bega kwa bega na walimu wa shule hiyo katika majukumu yao.
MWISHO.