Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
KATIKA Wiki ya Sheria inayoendelea katika Jiji la Dodoma na Dar es Salaam Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) inaendelea kutoa elimu kwa Bodi za Wadhamini zilizosajiliwa na RITA kufanya marejeo ya Katiba zao pamoja na kupata maelekezo ya kina kuhusu jinsi ya kufanya huduma hiyo kwa njia ya kielektroniki.
Kwa Dar es Salaam Maonesho ya Wiki ya Sheria yanaendelea katikaviwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam na Dodoma yanaendelea Nyerere square.
Akifafanua zaidi kwa waandishi wa habari Wakili wa Serikali Peter Mbogoro amesema kuwa bodi za wadhamini zilizosajiliwa na RITA zinatakiwa kufanya marejeo ya katiba zao kwa kufanya marekebisho ili kuboresha maeneo kama kuweka ibara inayoainisha chombo cha juu cha taasisi husika (Supreme Authority) kwa taasisi za kidini.
Pia kuweka ibara inayoelezea namna ya utatuzi wa migogoro inapotokea ndani ya taasisi, kuweka ibara inayoonesha muda wa ukomo wa wadhamini kukaa madarakani, kuweka ibara inayoonesha sababu za mdhamini/wadhamini kuondoka/kuondolewa madarakani, kuweka ibara inayoonesha idadi ya vikao vya wadhamini kwa mwaka na majukumu yake ikiwa pamoja na wajumbe wanaopaswwa kuhudhuria vikao husika na akidi (quoram) kwa vikao hivyo.
Aidha amesema taasisi zilizosajiliwa Ofisi ya Msajili na Jumuiya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na zinapaswa kusajili Bodi za wadhamini RITA lakini hazijafanya hivyo huku akitumia nafasi hiyo kuzitaka kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria. Pia bodi za wadhamini wa taasisi za kidini ambazo hazikusajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani zinaelekezwa kufanya hivyo.
Wakili Mbogoro amesema pia wanatoa elimu kwa umma kuhusu huduma za Wakala ikiwemo ya kuandika na kuhifadhi wosia ikiwa ni jitihada za kupunguza na kuondoa migogoro katika jamii, masuala yahusuyo mirathi ikiwa ni moja ya majukumu ya RITA kwa kuteuliwa na mahakama, masuala ya ndoa na talaka na pia tunasajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa.
Kwa upande wake Fatma Jumanne Mkazi wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam ameonesha furaha yake ya dhati baada ya kusajili cheti cha kuzaliwa na kupata elimu kuhusu ya masuala yahusuyo kuandika na kuhifadhi Wosia.
“Elimu ambayo nimeipata kuhusu shughuli zinazofanywa na RITA hasa ya kuandika na kuhifadhi Wosia itaniwezesha kuchagua msimamizi sahihi wa mirathi na hii itanisaidia kuepusha migongano katika familia yangu.”