Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Mheshimiwa Dkt. Mwinyi Haji Makame aliyewahi kuwa Muwakilishi wa Jimbo la Dimani na Waziri katika Wizara mbalimbali, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kilichotoke usiku wa kuamkia tarehe 20 Oktoba, 2022 nyumbani kwake Zanzibar.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndugu Samia Suluhu Hassan amemuelezea Marehemu Dkt. Mwinyi Haji Makame ni kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika uhai wake, kuleta maendeleo kwa wananchi na serikali kwa ujumla katika utumishi wake akiwa katika nyadhifa mbali mbali.
“Tumepoteza Kiongozi na Mwanachama muaminifu wa CCM aliyeitumikia nchi yetu kwa uadilifu, umakini na uhodari mkubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo ndani ya Chama na Serikali kwa vipindi vyote ambavyo alitumikia akiwa katika nyadhifa mbali mbali za utumishi wake” Ndugu Samia Suluhu Hassan
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatoa pole kwa familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa, Marafiki.
Marehemu Dkt. Mwinyi Haji Makame amekuwa Muwakilishi wa Jimbo la Dimani tokea mwaka 2000 hadi 2020 ambapo aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali na Chama Cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kuwahi kuwa Waziri wa Fedha na Mipango Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi Ameni.
Sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake Tutarejea.
Shaka Hamdu Shaka
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi
21 Oktoba, 2022