Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amekutana kwa mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Uhamiaji wa Ufalme wa Saudi Arabia Luteni Generali Suliman Al-Yahya katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na Mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na namna ya kukuza ushirikiano baina pande mbili ambapo Saudi Arabia imeonyesha utayari wa kujadiliana na Serikali ya Tanzania juu ya upatikanaji viza za kuingia nchini Saudi Arabia.
Kwa upande wake, Balozi Sokoine ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kutoa ushirikiano kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kijamii na kiuchumi.
Balozi Sokoine ametumia mazungumzo hayo kuelezea utayari wa Tanzania kuingia makubaliano ya kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya ushirikiano.