Mkurugenzi wa leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) Andrew Mkapa akizungumza wakati alipokuwa akifungua kikao kati ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA) pamoja na Taasisi za Sekta za Umma ili kupata maoni na mapendekezo ya Mabadiliko ya Sheria ya leseni za Biashara ya mwaka 1972.
Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Leseni za Biashara wa BRELA Tawi Kilemile akiwasilisha mada ya Mpendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Leseni za Biasara, sura 208 katika kikao cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheria ya leseni za Biashara, sura 208 Kilichofanyka leo Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Andrew Mkapa (katikati aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na kikosi kazi cha kuratibu ukusanyaji maoni ya wadau kuhusu marekebisho ya Sheia hiyo.
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Wakala wa usajili wa Leseni na Majina ya Biashara (BRELA) umezindua rasmi zoezi la kupokea maoni ya wadau juu ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya leseni za Biashara ya mwaka 1972.
Uzinduzi huo umefanyika leo Septemba 14,2022 Jijini Dar es Salaam ambapo wadau mbalimbali walikutana na kuipitia Sheria hiyo ili kufahamu maeneo gani katika sheria hiyo na kutoa mapendekezo yako ya marekebisho katika Sheria hiyo.
Akizungumza wakati wa kufungua rasmi zoezi hilo Mkurugenzi wa leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Andrew Mkapa amesema kuwa kupitia kikao hicho kutawezesha kupata mchango utakaofanikisha maboresho ya Sheria hiyo ili kuifanya iendane na mazingira ya sasa ya kufanya biashara pamoja na kanuni mbalimbali zinazopaswa kufanyiwa marekebisho.
“kupitia kikao hiki kutawezesha kupatikana kwa michango itakayofanikisha maboresho ama marekebisho ya Sheria ya leseni za Biashara Sura 208 ambayo imeonekana kupitwa na wakati”
“Sheria iliyopo kwa sasa haiendani na mazingira ya wakati huu na imeonekana kuwepo na mikwamo kadhaa kutokana na Mabadiliko ya Teknolojia ya Ufanyaji Biashara ikiwemo Biashara za mtandaoni ambazo Sheria hii haiwagusi kabisa”amesema Mkapa.
Ameongeza kuwa mkutano huo utadumu kwa siku tatu na kupokea maoni kutoka kwa wadau wa Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi kisha kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu kijaji juu ya mchakato huo watakaa na kuyachakata maoni hayo ili kupata sheria inayokidhi matakwa ya wote.
Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara (WUVB) Denis Mzamiru amesema kinachowasukuma kufanya maboresho na Marekebisho ya Sheria hiyo ni pamoja na kuifanya Sheria kuendana na Mazingira ya sasa ya ufanyaji Biashara ikienda sambamba na uwepo wa urahisi na wepesi kwa wafanyabiashara kupata leseni za Biashara.