NA: HERI SHAABAN
Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, ameipongeza Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo kwa jitihada zake za kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto na kuwataka wadau wengine kuiunga mkono.
Kumbilamoto aliyasema hayo katika wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyoandaliwa na taasisi ya Fahari na kufanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ulongoni.
Alisema ukatili unatokea kwa sababu watu wengi hawana hofu ya Mungu na kuwataka wazazi na walezi kumrudia Mungu.
“Kama ingekuwa waislam wanafuata maandiko, wakristo wanafuata maandiko ukatili usingetokea katika taifa letu kwa sababu maelekezo ya dini zote yanakataa kuwafanyia watoto ukatili,” alisema Kumbilamoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo, Neema Mchau, alisema katika kuadhimisha siku hiyo waliguswa pia kutoa msaada kwa watoto 100 wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaosoma katika Shule za Msingi Ushindi na Ulongoni.