TMDA
Home BUSINESS WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UJENZI BANDARI YA UVUVI KILWA

WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UJENZI BANDARI YA UVUVI KILWA

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mhe. Mashimba Ndaki (kushoto) eneo  ambalo limetengwa kwa ajili ya kujenga Bandari ya Uvuvi lililopo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi. Waziri Ndaki alitembelea eneo hilo Mei 27, 2022 kwa lengo la kulikagua kabla ya ujenzi kuanza rasmi. Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Ndaki alisema Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ambao utaanza mapema mwezi Juni.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainab Kawawa (kulia) akimpatia maelezo Mhe. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) kuhusu maeneo ambayo wananchi wapo tayari kuyaachia ili kupisha mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi itakayojengwa Wilayani humo kuanzia mapema Mwezi Juni. Waziri Ndaki alitembelea eneo lililotengwa kujenga Bandari hiyo Mei 27, 2022.


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na Wananchi wa Kilwa hawapo pichani muda mfupi baada ya kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi lililopo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi Mei, 27, 2022. Akiongea na Wananchi hao ambao wengi wao ni Wavuvi aliwahimiza kujiandaa na fursa mbalimbali zitakazojitokeza kutokana na utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo ili waweze kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao

Na:Mbaraka Kambona, Kilwa,

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Wananchi hususan wanaoishi wilayani Kilwa kuhakikisha wanajipanga  kutumia vyema fursa zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ambao ujenzi wake utaanza mapema Mwezi Juni mwaka huu.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua eneo
ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo ya uvuvi lililopo
Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi Mei 27, 2022.

Wakati akizungumza na Wananchi wa wilaya hiyo alisema, kuanza kwa ujenzi wa mradi huo kutaambatana na fursa mbalimbali ambazo zitakuwa na manufaa kwao hivyo ni vyema wananchi hao wakaanza kujiandaa ili mradi utakapoanza nao waweze kuwa sehemu ya wanufaika na sio watazamaji Aliongeza kwa kusema kuwa katika kuhakikisha mradi huo unajengwa na kukamilika, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kutengwa kiasi cha pesa kisichopungua bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo.

“Naomba muiamini Serikali ya Mama yetu makini, Rais Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kuijenga Tanzania, huu ni mradi wake wa kielelezo, wakimkakati na utakaoacha alama kwenye nchi hii,” alisema.

Waziri Ndaki aliwahakikishia Wananchi wa Kilwa  kuwa bandari hiyo itaanza kujengwa hivi mapema Mwezi Juni mwaka huu na hivyo aliwataka kujiandaa kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza wakati mradi huo unatekelezwa.

Awali, akitoa taarifa ya namna Wilaya ilivyojiandaa kuhakikisha mradi huo unajengwa, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Zainab Kawawa alisema kuwa wameshafanya matayarisho yote kuhakikisha mradi huo unajengwa huku akiongeza kuwa wananchi ambao wanakiwa kuachia maeneo yao kupisha mradi huo wapo tayari kufanya hivyo.

“tunaamini kwamba bandari hii ya kimkakati itakapojengwa na kukamilika italeta tija kubwa kwa wavuvi na wananchi kwa ujumla, na sisi tumeshafanya matayarisho yote ili mradi huu usikwame,” alisema.

Naye, Mwananchi na Mvuvi anayefanya shughuli zake Wilayani Kilwa, Bw.
Suleiman Mohammed akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema ni kweli wanavuna samaki katika bahari ya Hindi lakini hawana sehemu ya uhakika ya kuuzia Samaki wao kwa kuwa soko lililojengwa kwa ajili ya shughuli hiyo mpaka leo halijaanza kutumika.

“Tunakuomba Mhe. Waziri soko hili lililojengwa lifanye kazi ili tuweze kulitumia kufanya biashara zetu,” alisema Mohammed. 

Aidha, Waziri Ndaki aliwataka wananchi ambao wanatakiwa kuachia maeneo yao
kwa ajili ya kupisha mradi huo wasiwe na wasiwasi,  Serikali itahakikisha kila mmoja anapata haki yake anayostahili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Open chat
GREEN WAVES MEDIA
Ahsante kwa kutembeiea WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UJENZI BANDARI YA UVUVI KILWA