Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania Nchini Malawi Mheshimiwa Balozi Humphrey Polepole, Mazungumzo yaliofanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais mkoani Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania Nchini Malawi Mheshimiwa Balozi Humphrey Polepole mara baada ya kumaliza mazungumzo yaliofanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais mkoani Dodoma.
DODOMA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania Nchini Malawi Mheshimiwa Balozi Humphrey Polepole. Mazungumzo hayo yamefanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais amempongeza huyo kwa kuteuliwa na imani aliopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa nchini Malawi. Makamu wa Rais amemsihi Balozi Polepole kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya taifa.
Makamu wa Rais amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi hivyo amemtaka Balozi Polepole kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.
Amesema nchi za Afrika zina uwezo wa kufanya uwekezaji baina ya mataifa yao na kupata manufaa makubwa hivyo amemsihi Balozi Polepole kuvutia wawekezaji wa Malawi hapa nchini pamoja na kutafuta fursa za uwekezaji nchini Malawi.
Aidha amemuasa kutambua vipaumbele vya taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi zilizopo katika Dira ya taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na vipaumbele vilivyopo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.
Halikadhalika amemuagiza Balozi Polepole kuhakikisha anashiriki katika mikutano mbalimbali itakayowezesha kujifunza, kueleza mazuri ya Tanzania pamoja kuvutia wawekezaji. Amesema ni muhimu kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo ikiwemo kutafuta fursa ya kufundishwa kwa lugha hiyo nchini Malawi.
Aidha amemuasa kuwaunganisha watanzania wanaoishi nchini Malawi ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.
Makamu wa Rais amemsihi Balozi Polepole kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zinazopelekwa katika kuendesha ubalozi huo ili kuongeza tija ya uwakilishi nchini humo.
Kwa upande wake Balozi Humphrey Polepole amemshukuru Makamu wa Rais kwa miongozo aliompa na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya taifa la Tanzania. Amesema tayari ameanza kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo zinazoweza kutatuliwa kupitia mamlaka za Tanzania kama vile Bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).