Home LOCAL VIJIJI VYA LIPALWE A, B KUNYWA MAJI SAFI, SALAMA

VIJIJI VYA LIPALWE A, B KUNYWA MAJI SAFI, SALAMA

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba, Mhandisi Ndolimana Kijigo akimkabidhi koki Mkandarasi wa Mradi wa Maji Lipalwe A na B, Mhandisi Anold Leopard.


Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tandahimba, Mhandisi Ndolimana Kijigo akimuelekeza fundi anayejenga banio la maji la Mradi wa Maji Lipalwe A na B (2)

Na: Selemani Msuya, Tandahimba

BAADA ya miaka 60 ya wananchi wa vijiji vya Lipalwe A na B kata ya Mahuta wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kutoshuhudia maji yakitoa bombani, hatimae Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani humo, imetumia Sh. milioni 470 kufikisha maji katika vijiji hivyo.

Hayo yamethibitishwa na Meneja wa RUWASA wilayani Tandahimba, Mhandisi Ndolimana Kijigo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea Mradi wa Maji Mahuta ambao utanufaisha zaidi ya wanakijiji 2,900 wa vijiji vya Lipalwe A na B.

Mhandisi Kijigo amesema mradi huo wa maji unaogharimu Sh.milioni 470, unatekelezwa na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kupitia fedha za mkopo usio na riba Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Amesema ujenzi wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 80 na matarajio yao ni ifikapo mwisho mwa mwezi Mei, 2022 wananchi waweze kuchota maji bombani safi na salama.

“Hapa Lipalwe A na B wana zaidi ya miaka 60 yaani tangu tupate uhuru hawajaona maji ya bomba ila RUWASA tumefikisha maji bombani. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa kuleta fedha za mradi wa maji safi na salama hapa Lipalw,” amesema.

Meneja amesema mradi huo utahusu ujenzi wa banio ambalo litagharimu zaidi ya Sh.milioni 30, matenki mawili moja lina uwezo wa kujaza lita 25,000 na lingine lita 50,000.

Kijigo amesema mkandarasi amefanya kazi ya kuchimba mtaro, kutandika mabomba kwenye vijiji vyote na kujenga vituo saba vya kuchotea maji

“Mradi huu ukikamilika wananchi 2,900 wa Lipalwe A na B watapata maji safi na salama. Tuna uhakika kasi hii ya ujenzi wa miradi ya maji, itafanikisha Tandahimba kufikia asilimia 85 ya upatikanaji maji vijiji mwaka 2025,” amesema.

Mhandisi Kijigo amesema, pamoja na miradi huo unaotekelezwa kwa fedha za ustawi pia RUWASA Tandahimba wanatekeleza miradi ya Maji  Mkwiti unaogharimu Sh.bilioni 6.4, Nanyula Maundo wa Sh.bilioni 4.2, Nanyanga Sh.milioni 230, Tukuyu  na Mdimba Sh.milioni 337.

Mhandisi huyo amesema pia kuna mradi wa National Water Fund unaogharimu Sh.bilioni 8.5, hivyo Tandahimba kwa mwaka ujao watakuwa na vijiji zaidi y 51 ambavyo vitakuwa havina huduma ya maji, kuhu upatikanaji maji safi na salama ukifikia asilimia 71.2.

“Hali ya upatikanaji maji Tandahimba ilikuwa imeshuka hadi asilimia 46 lakini kupitia huu mradi wa huu na mingine  asilimia itaongezeka na lengo la kufikia asilimia 85 mwaka 2025 litatimia,” amesisitiza.

Kwa upande wake Mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Anold Leopard  kutoka Kampuni ya Alem Construction Limited amesema anashukuru kupata nafasi ya kutekeleza mradi huo na kwamba hatamuangusha Rais Samia na Serikali.

Amesema mradi una changamoto kidogo lakini wamekuwa wakizipatia ufumbuzi kwa kushirikiana na RUWASA.

“Tunashukuru kupata mradi huu, tupo kwenye hatua za mwisho za utekelezaji, tumefikia asilimia 80, naamini tutamaliza kwa wakati, pamoja na changamoto ya ujenzi wa banio, hasa kwenye kufikisha vifaa na mitambo ya ujenzi,” amesema.

Mkandarasi huyo amesema uamuzi wa Serikali kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa kutekeleza miradi hiyo ya majii ni cha kupongezwa na wao watahakikisha hawawaangushi.

Amesema katika mradi huo wameweza kutoa ajira za nafasi mbalimbali kwa zaidi ya watu 40 jambo ambalo limewezesha shughuli za kiuchumi kuongezeka.

“Namwambia Rais Samia aendelee kuchapa kazi, kazi iendelee na sisi Wakandarasi wa ndani hatutamuungusha. Tutatekeleza miradi kwa ufanisi mkubwa,” amesisitiza.

Wakizungumza na mwandishi wanavijiji, Sulum Hamis, Josephine Uledi na John Sangwale wamesema walikuwa hawaamini kuwa ipo siku watachota maji bombani, ila kupitia Rais Samia na RUWASA hatimaye wameshuhudia.

Wamesema kwa miaka zaidi ya 60 wamekuwa kijijini hapo wakiomba kupatiwa maji kama Watanzania wengine, lakini ilishindikana, hivyo ujio wa RUWASA wanaona wamezaliwa upya.

Naye Meneja wa RUWASA Mkoa wa Mtwara, Primy Damas amesema mkoa huo unatekeleza miradi ya ustawi katika majimbo tisa ambapo hadi sasa wamefikia asimilia 50 ya utekelezaji.

“Mkoa huu una wilaya tano ambapo miradi ya ustawi inatekelezwa majimbo mawili ya Wilaya ya Mtwara ambayo ni Nanyamba na Mtwara DC, Newala mawili, Masasi matatu, Nyanyumbu na Tandahimba kuna majimbo mawili.

Miradi hii tisa inagharimu Sh.bilioni 5.37 na ikikamilika itaweza kuhudumia watu 65,000 na kuongeza asilimia ya upatikaji maji kuwa asilimia sita, hivyo tutatoka asilimia 62 ya upatikanaji maji hadi asilimia 68,” amesema.

Mhandisi Damas amesema pia wanatekeleza miradi ya lipa kwa matokeo chini ya mfuko wa maji ambayo pamoja na miradi mingine ikikamilika watafikia asilimia 75 ya upatikanaji wa maji.

Meneja huyo alisema pia kupitia mipango mbalimbali ya mkoa na wizara wanatarajia kupitia mwaka wa fedha 2022/2023 hadi 2025 lengo la maji vijijini asilimia 85 litafikiwa.

Mhandisi huyo ametoa wito kwa wananchi ambao miradi inatekelezwa katika vijiji vyao kutunza miundombinu hiyo ili iwe endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Previous articleBARRICK YADHAMINI KONGAMANO LA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU
Next articleWAKRITO WATAKIWA KUONESHA MATENDO YA HURUMA NA KUTOA SADAKA KWA MAKUNDI YA WATU WENYE UHITAJI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here