Na: Mwandishi Wetu- Dar es salama
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe.Balozi Dkt.Pindi Chana amewataka waraibu wa dawa za kulevya kutumia fursa za kliniki za kuponya zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kurejea katika hali ya kawaida kushiriki katika shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa.
Mheshimiwa Pindi ametoa rai hiyo Jijini Dar es salam baada ya kufanya ziara katika Kliniki ya Methadone iliyopo katika Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala ambapo inasimamiwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).
Pia aliishauri idara hiyo kushirikiana bega kwa bega na idara nyingine vikiwemo vitengo vilivyopo halmashauri kama Mwanasheria wa Halmashauri ili pale ambapo kuna uhitaji aweze kushiriki kikamilifu kutoa huduma.
“Niwasishi watu wote mnapata dawa hizi saidizi hususani methadone muendelee kuzitumia kadri mnavyoelekezwa ili kuepuka changamoto ya kurejea katika hali za awali iwapo mtasistisha kuzituma kwa sababu Serikali inatamani kuona kila mwananchi anafanya kazi halali kujiingizia kipato maana kuendelea kuzitumia unaharibu afya yako na kupunguza nguvu kazi ambayo ni vijana,” alisema Mhe. Pindi.
Pia aliwataka maafisa ustawi wa jamii kuwahamasisha vijana hao kujiunga katika vikundi ili waweze kunufaika kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau wengine nchini baada ya kupona kwani Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa, vijana wote wananufaika kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Hata wale wenye changamoto, waraibu wanayo haki ya kujiunga katika vikundi wakapata fursa hii, na mikopo hii inatolewa pasipokuwa na riba ya aina yoyote. Hizi ni jitihada za Serikali yetu za kuwasaidia wanawake na vijana, hivyo fursa hizi zinatolewa katika vikundi, ni muhimu sana vijana wakajiunga katika vikundi, kwani umoja ni nguvu. Kikundi chenye ndiyo dhamana, ya kurudisha fedha hizo ili wengine wapate.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dkt. Zavery Benela alieleza kwamba , Kliniki ya MAT, Mwananyamala inahudumia wateja zaidi ya 1,350 kila siku ambao wanafika kupata huduma.
Kwa upande wake Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Dkt. Peter Mfisi alifafanua kwamba hadi Desemba mwaka jana zaidi ya waraibu 10,600 walikuwa wamehudumiwa kupitia vituo vya tiba saidizi kwa waraibu, vikubwa kwa vidogo vilivopo hapa nchini.
“Kwa sasa tuna vituo 15 ambapo kuna vinne vidogo huku 11 vikiwa vikubwa kwa ajili ya kutoa tiba saidizi kwa waraibu kwa kutumia dawa.Vituo hivi husimamiwa na Serikali na huhudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya na waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu,” Alifafanua Dkt.Mfisi.
Akieleza baadhi ya sababu zinazisababisha vijana wengi kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya Afisa Ustawi wa Jamii anayesimamia kliniki hiyo, Hafsa Mtwange alitaja kuwa ni pamoja na makundi, hali ya maisha na ndoa.
Vilevile Mtaalamu kutoka Kliniki ya MAT Mwananyamala, Dkt. Miriam Kabanywanyi alibainisha kuwa, wamekuwa na jukumu kubwa la kuwajenga kisaikolojia waraibu hao wa dawa za kulevya, kwani kila anayefika kituoni hapo ana changamoto zake kubwa ikiwa ni kuathirika kisaikolojia.
“Hivyo, tunatumia muda mwingi kuwajengea uwezo kwa kuwaandaa kisaikolojia ili waweze kuyakubali mazingira ya kupatiwa tiba na baada ya kuhitimu waweze kuwa watu mwema katika jamii na kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao na jamii kwa ujumla,”alieleza Dkt. Miriam.
Aidha baadhi ya waraibu walieeleza kuwa, changamoto kubwa ambazo wanakabiliana nazo baada ya kuhitimu hatua hiyo ya kupatiwa dawa na kurudi katika hali ya kawaida ni pamoja na kukosa kazi za kufanya, hivyo kujikuta wanajiingiza tena kwenye makundi mabaya.
MWISHO