NA: MWANDISHI WETU.
MDHAMINI mwenza wa Ligi Kuu ya Wanawake (Tanzania Serengeti Lite League) Rani Sanitary Pads imetoa zawadi ya taulo za Kike (Pedi) kwa timu ya Yanga Princes jana katika pambano la timu hiyo dhidi ya JKT Queens lililochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na Yanga Princes wakishinda mabao 3-1.
Rani Sanitary Pads inayojihusisha na uzalishaji wa taulo hizo imepanga kutoa taulo hizo kwa timu zote 12 zinazoshiriki ligi hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Rani Sanitary Pads Ramadhan Badi alisema wamekuwa na utaratibu wa kutoa maboksi sita ya taulo kwa kila timu ili kuondoa changamoto ya wachezaji kikosini.
Alisema mpaka sasa wameshatoa kwa timu mbalimbali na zoezi hilo litaendelea kwa timu nyingine.
“Tumefurahi kuwa sehemu ya wadhamini wa ligi yetu ya kina mama msimu huu, kama taasisi tuna mengi mazuri ambayo tunayo, lakini mwanzo wetu ni huu wa kuzipa timu zote shiriki bidhaa zetu.
“Mpira wa kina mama una changamoto nyingi, tunaamini uwepo wetu unaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuvutia na watu wengine kuweza kuwekeza katika mpira huu” alisema Ramadhan.
Mpaka sasa Rani Sanitary Pads imeshagawa taulo hizo kwa timu za Simba Queens, JKT Queens, Ruvuma Queens, Oysterbay Queens na leo jioni itaenda kuipa timu ya Ilala Queens katika pambano lake la ligi hiyo dhidi ya Simba Queens katika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.