DODOMA.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashantu Kijaji (Mb) amesema Serikali imeanzisha Kongani ya Viwanda Dodoma itakayokuwa na viwanda vitakavyotumia malighafi zinazozalishwa nchini ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hasan katika uanzishaji wa kongani za viwanda.
Dkt Kijaji amayasema hayo katika Hafla fupi ya makabidhiano ya eneo maalum la uwekezaji (SEZ) lenye ukubwa wa hekari 1500 katika eneo la viwanda Nala lililotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji na Mauzo ya Nje (EPZA), iliyofanyika jijini Dodoma Januari 20, 2022.
“Kongani hii itumike kuhudumia Kanda ya kati kwa kuwa na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo hususan Alizeti inayolimwa Dodoma, Singida na Simiyu ili kuwa na mafuta ya kula ya kutosha mahitaji ya ndani na kuuza nje ya nchi na kutumia Reli ya Kisasa ya SGR kwa kusafirisha mizigo kwenda masoko ya nje ya Nchi ipasavyo.” Amesema Waziri Kijaji.
Waziri Kijaji pia amezielekeza Taasisi za EPZA na TIC kushirikiana kwa karibu na Sekta Binafsi pamoja na Uongozi wa Mkoa wa Dodoma ili kuhakikisha kongani hiyo inaendelezwa kwa wakati ili kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita katika uanzishaji, uendelezaji na uwekezaji wa kongani za viwanda nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Antony Mtaka akimkaribisha Waziri amesema Maeneo ya EPZA yanavutia wawekezaji hivyo Ofisi yake iko tayali kishirikiana na Wizara katika kuhakikisha miundombinu muhimu kama Maji, Umeme na Barabara inapatikana ili kukamilisha ujenzi wa kongani hiyo kwa wakati na kuvutia wawekezaji na hivyo kuleta maendeleo Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof.Godius Kahyrara amesema ni muhimu EPZA kutenga maeneo ya kongani za kiuchumi zenye hadhi ya kimataifa kwa kuzingatia wawekezaji wadogo zinazolenga kutoa ajira nyingi ili kutimiza Malengo ya Serikali katika kiongeza ajira na pato la Taifa kwa ujumla.
” EPZA tengeni kongani maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya uzalishaji bidhaa za ujenzi ili kutosheleza mahitaji ya vifaa hivyo nchini na kuondokana na uagizaji wa vifaa hivyo nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa EPZA Bw. Charles Itembe akitoa taarifa kwa Waziri amesema eneo Hilo lililotengwa linatarajiwa kuwa kitivo maalumu cha uwekezaji katika nyanja mbali mbali kama vile ununuzi,usafirishaji, kilimo, ujenzi, madinj, nguo na madawa na kutoa ajira takriban 100,000.
Awali, Afisa Mipango mini wa mkoa wa Dodoma akitoa taarifa anesema Mkoa unetenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo katika eneo la Nala hekari 2285 zimetengwa ambapo hadi sasa hekari 300 zimegawiwa kwa wawekezaji wa nje, 1500 kwa EPZA, na 21 kwa wawekezaji wazawa.