Na:Heri Shaaban
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu David Kafulila, ameagiza wazawa wa Malampaka wapewe kipaumbele kwenye ajira ya Ujenzi wa reli ya kisasa ( SGR), Mwanza/ Isaka.
Mkuu wa Mkoa Kafulila alitoa maagizo hayo katika mkutano wa hadhara Wilayani Maswa wakililia wapate ajira katika mradi wa SGR kutoka Mwanza Kwenda Isaka uliondaliwa na Mkuu wa mkoa kwa ajili ya kusikiliza malalamiko yao kuhusu kubaguliwa kwao katika masuala ya ajira pamoja na kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwenye mradi huo uliofanyika mjini Malampaka.
Wananchi hao walimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa wakati mradi huo unatambulishwa kwa mara ya kwanza kwao na viongozi wa serikali walielezwa kuwa wakazi wa eneo hilo ambapo panajengwa bandari ya nchi kavu watapatiwa kipaumbele kwenye masuala ya ajira.
“Ninaagiza kwa vyombo vya dola kufutailia suala la rushwa kama lipo na kutaka wahusika watakaobainika kuchukuliwa hatua za kusheria katika mradi huu wa SGR ” alisema Kafulila .
Kafulila aliagiza kupelekewa majina ya watu walioajiriwa kama wanatoka mkoa wa Simiyu au la kwani serikali imekuwa ikitaka wanufaika wa kwanza wawe wanaoishi kwenye eneo la mradi wanatoka eneo husika sio nje ya Mkoa huo.
Awali katika mkutano huo kwa upande wake Juma Lufuta alisema mwanzoni walielezwa mradi utakapoanza kipaumbele kitatolewa kwa wananchi ambao wanaishi katika eneo ambalo mradi unatekelezwa lakini cha kushangaza mambo yamekwenda kinyume kabisa wengi wa waajiriwa wanatoka nje kabisa ya mkoa wa Simiyu.
Juma alisema katika ajira wamekuwa wakibaguliwa jambo baya zaidi katika kupata ajira hizo vitendo vya rushwa vimeshamiri sana.
Alisema kuwa licha ya kufuatilia na kutoa malalamiko yao kwa viongozi wa Shirika la Reli Nchini(TRC)walioko kwenye eneo hilo wamekuwa wakijibiwa kuwa hawana sifa jambo ambalo wamedai kuwa si kweli.
Fatuma Saidi alisema hata ajira ya kushika kibendera vya kuonyesha gari ipite au isipite kuna kazi inaendelea unakuta mtu anatolewa Dar Es Salaam je kwa mji wa Malampaka au mkoa mzima wa Simiyu hawapo watu wenye uwezo huo, napo panahitaji sifa ya namna gani?,”alihoji
Kwa upande wake Naibu Meneja Mradi wa TRC,Mhandisi Alex Bunzu alisema kuwa malalamiko ya ajira za upendeleo na baadhi ya wafanyakazi wa mkandarasi kuomba rushwa ili watoe ajira kwa wananchi yameshafanyiwa kazi.
‘Malalamiko haya haya tumeshayafanyia kazi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali wafanyakazi waliohusika wameondolewa kwenye ajira na tunaendelea kufuatilia kwa ukaribu tuhuma za rushwa na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria,’alisema.
MWISHO