Home LOCAL WIKI YA KAMPENI YA USAFI KUZINDULIWA MARA

WIKI YA KAMPENI YA USAFI KUZINDULIWA MARA

Na: Mwandishi wetu, MARA.

MKOA wa Mara unatarajiwa kuzindua Wiki ya Kampeni ya Usafi wa Mazingira, Kesho asubuhi ambayo ni mwendelezo wa mpango uliyoasisiwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipokuwa Makamu wa Rais.

Uzinduzi huo kimkoa utaanzia kwenye Stendi ya mabasi, katikati ya Mji wa Musoma Saa 1:00  asubuhi ukiongozwa na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Mkoa huo, Ally Hapi.

Akizungumza na Vyombo vya Habari ndani ya Ikulu ya Mkoa huo Leo, RC Hapi alisema wakati shughuli hizo zikiendelea mjini Musoma wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote Tisa za Mkoa huo nao watakuwa wakifanya uzinduzi katika mazingira yao.

Amesema yeye pamoja na watumishi wa serikali, taasisi, mashirika, makampuni na vyombo vyote vya ulinzi na usalama watashirikiana na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya Mji wa Musoma kufanya usafi.

Ametaja baadhi ya maeneo watakayoyafikia kuwa ni Stendi ya zamani, Soko kuu la mjini, Nyasho na Soko la Nanenane.

Kampeni hiyo itafanyika wiki nzima na baadaye kila Juma mosi asubuhi kila mtu atatakiwa kusafisha mazingira ya nyumbani kwake na anakofanyia  kazi kabla ya kuendelwa na mambo mengine.

Hatua hiyo imefuatia ziara ya kikazi iliyofanywa na RC Hapi kwenye halmashauri zote na kubaini kukithiri kwa uchafu wa mazingira.

Alisema hata jitihada za serikali kuboresha miundombinu ikiwamo kujenga mitaro kandokando ya barabara haitaleta tija endapo wanaoishi au kufanya shughuli pembezoni mwa mitaro hiyo hawataisafisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here