Na: Muhidin Amri, Namtumbo.
WAKULIMA wa zao la Tumbaku katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wamelalamikia makato ya asilimia 2 yaliyofanywa na Serikali kupitia Mamlaka ya mapato Nchini (TRA) katika msimu wa kilimo 2021.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao jana, wakulima wa Tumbaku kutoka Chama cha Msingi cha Suruti(Suruti Amcos) wameshangazwa na hatua ya Serikali kuwakata fedha kwa kila kilo moja ya tumbaku bila kuwashirikisha wakulima ambao ndiyo wanaotumia nguvu na gharama kubwa katika uzalishaji.
Shami Ponera amesema,tozo ya asilimia mbili kwa kila mkulima sio sahihi kwani Serikali tayari imeshakata kodi yake kupitia Chama Kikuu cha Ushirika cha Namtumbo na Songea (Sonamcu).
Amesema, hatua hiyo ni sawa na uonevu mkubwa kutokana na unyonge wao, kwani haiwezekani hata kidogo wakulima wakatwe tozo mara mbili na kuiomba Serikali iangalie suala hilo upya kwani linawaumiza sana wakulima.
Kwa mujibu wa Ponera,zao la Tumbaku ni gumu katika uzalishaji wake kwa kuwa linachukua takribani miezi tisa tangu hatua ya awali hadi linapofikiswa sokoni, kwa hiyo ni vizuri Serikali ikaangalia upya juu ya tozo hiyo ambayo inawakandamiza na kuwarudisha nyuma wakulima wa zao la Tumbaku.
Ameiomba Serikali, kuhakikisha inarudisha fedha ilizochukua kwa wakulima ili ziweze kuwasaidia kujiandaa na msimu mpya wa kilimo kwa kuwa ni haki yao ya msingi, na Serikali haijatoa msaada wowote kwa wakulima wakati wa maandalizi ya zao hilo.
Mkulima mwingine Ali Chemka amesema, suala la tozo ya asilimia mbili kwa mkulima wa Tumbaku halikufanyika kwa haki kwani serikali ilitakuwa kuwataarifa kwanza kwakulima kabla haijaanza kukata tozo hiyo ili kuona uhalali wake.
Chemka ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SonamcuLtd) amesema, tozo hiyo imeleta mgogoro mkubwa kati ya wakulima na uongozi wa Sonamcu na kuiomba Serikali itumie hekima na busara na kurudisha fedha ilizochukua kwa wakulima.
“Mimi sikatai kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, hata hivyo ninachoomba ni muhimu sana kuwepo na mawasiliano kati ya mlipa kodi(mkulima) na serikali badala ya maamuzi hayo kufanywa na upande mmoja”amesema Ponera.
Amesema,wakulima wa Tumbaku wanakabiliwa na changamoto nyingi katika
uzalishaji wa Tumbaku, kwa hiyo ni vyema serikali iangalie upya suala hilo ambalo kimsingi linawarudisha nyuma wakulima.
Chemka amesema, baadhi ya wakulima wana madeni makubwa ya fedha walizochukua kutoka katika taasisi za fedha na kwa watu binafsi ambazo wanategemea kulipa baada ya kuuza Tumbaku kwa hiyo hatua ya Serikali ya kukata fedha kina hatarisha maisha na usalama wa wakulima.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Sonamcu Juma Mwanga amesema,kodi ambayo Serikali imewatoza wakulima katika msimu wa kilimo 2020/2021 imekuja ghafla na Serikali haikustahili kukata kodi ya asilimia mbili kwa wakulima.
Mwanga amesema, kisheria tozo hiyo inatakiwa kukatwa pale wakulima wanapouza Tumbaku kwa makampuni na watu binafsi siyo wanapouza kwa Chama cha Ushirika.
Mwanga ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo kupitia upya sheria hiyo hususani kwa zao la Tumbaku ambalo uzalishaji wake unakabiliwa na changamoto kubwa na ni vyema kodi hizo zielekezwe kwenye mazao mengine badala ya Tumbaku.
Ameshangazwa na hatua ya Serikali kuwakata wakulima asilimia mbili, wakati Sonamcu kama chama cha wakulima wa Tumbaku imeshalipa Dola za Marekani zipatazo 13 sawa na Sh. Milioni 32.
Amesema,ni makosa kuwakata tozo wakulima wanaouza Tumbaku yao kwa vyama vya Ushirika kwani sheria ya kodi ya mwaka 2021 inataka mkulima kulipa kodi pale atakapouza Tumbaku kwa makampuni au watu binfasi na sio kwa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika.
Aidha ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo na wizara ya fedha, kukaa na kutafsiri upya sheria hiyo kama vyama vya msingi na vyama vya ushirika vinastahili kukatwa tozo hiyo.
Amesema wakulima hawakatai kulipa kodi, lakini Serikali ilitakiwa kukaa na wadau ili kujadili na kutoa elimu kabla haijaanza kukata kodi hiyo ili kupata maoni.
Kwa mujibu wa Mwanga, kama itaendelea kushikilia msimamo wa kukata tozo kwa wakulima basi kuna uwezekano mkubwa wa kushuka kwa uzalishaji wa Tumbaku katika msimu wa kilimo 2021/2022.
MWISHO.