Na: Paul Zahor, GEITA, RS.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule ameiagiza Halmashauri ya Mji Geita ndani ya siku saba kuanza kufanya ukarabati wa Stendi ya Mabasi Mjini Geita ili iwe na Mazingira rafiki kwa watumiaji ikiwa ni pamoja na Maegesho, vifaa vya kuwekea takataka na Mifereji ya maji kwa kuzingatia wakati wa masika unakaribia.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo Septemba 13, 2021 wakati alipozuru kwenye Stendi hiyo kusikiliza kero za wananchi na ndipo alipofanya Mkutano na wafanyabiashara na wasafirishaji kwenye Stendi hiyo.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameagiza kuanza haraka kwa taratibu za Ujenzi wa Stendi mpya kama vikao na kutafuta mkandarasi ili ijengwe mapema iwezekanavyo kutokana na umuhimu wake kwa wakati huu.
“Ndugu viongozi twendeni tukajenge Stendi Mpya kama Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anavyotaka Mambo yaende kwa viwango lakini kwa speed na sio kusubiri subiri.” Amesisitiza.
“Mhe. Rais ametoa Bilioni 100 kwa ajili ya kuleta Maji kutoka kwenye ziwa Viktoria na itakapokamilika Miradi hii basi moja kwa moja suala la maji hapa Geita itakua historia, aidha tunashukuru sana kwa Bilioni 7 alizotupatia kwenye kila jimbo Mkoani Geita kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya Barabara kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA).” Amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe. Simon Shimo amekemea vikali tabia ya watoto kufanya Shughuli za biashara kwenye Stendi na ametoa wito kwa Viongzi wa Stendi kuhakikisha wanazuia suala hilo lisitokee.