Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti (katikati) akiwa na wajumbe wa Kamati ya Usalama Mkoa huo walipokagua kiwanda cha kuzalisha unga cha Mbasira Food Ltd. Imeelezwa kuwa kinazalisha tani 100 za unga wa sembe na dona kwa siku mjini Sumbawanga hivyo kuwa soko la mahindi la uhakika.
(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Joseph Mkirikiti amekipongeza kiwanda cha kuzalisha unga cha Mbasira Food Ltd cha Sumbawanga kwa kuanza kutoa fursa ya upatikanaji wa soko la uhakika la mahindi ya wakulima.
Kiwanda hicho kinachomilikiwa na watanzania wazalendo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake Ramadhani Balukuli kina uwezo wa kukuzalisha tani Mia Moja za unga wa sembe na dona kwa siku ambapo kimeajili watu Mia Moja hadi sasa.
Mkirikiti amesema hayo hivi karibuni alipofanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya kiwanda hicho kilichopo eneo la Malangali Manispaa ya Sumbawanga ambacho kilishindwa kufanyia kazi kwa muda wa mwaka mzima kutokana na deni la umeme toka Tanesco.
“Uwepo wa kiwanda hiki kikubwa kwenye mkoa wa Rukwa ni fursa ya uhakika wa soko la mahindi ya wakulima wetu, hivyo nataka kuona wawekezaji hawa wanapata ushirikiano ili wazalishe ajira za kutosha” alisisitiza Mkirikiti aliyefuatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwasihi wamiliki wa kiwanda hicho kufanya kila jitihada kiwanda kisifungwe tena kama ilivyokuwa awali kilipokuwa kikifahamika kwa jina la Barka Milling Limited kwa kuwa na deni ya umeme serikali imeweka utaratibu mzuri wa mwekezaji kulipa huku akiendelea na huduma.
Akitoa maelezo ya kiwanda hicho, Mkurugenzi Mtendaji wake Ramadhan Balukuli alisema yeye pamoja na wenzake wamenunua kiwanda hicho toka kwa kampeni ya kigeni ya Barka Milling Limited hapo mwaka 2020 kufuatia mkopo wa fedha Dola za Kimarekani Milioni 1.5 toka Benki ya SFC Finance ya Mauritius baada ya kupata usimamizi toka Benki ya kizalendo ya Azania ya Tanzania.
Balukuli aliongeza kusema kiwanda hicho kina mtaji wa Dola za Kimarekani Milioni 2.5 sawa na Shilingi Bilioni 5.85 kwa ajili ya kununua mahindi toka kwa wakulima wa mkoa wa Rukwa, Songwe na Ruvuma ambapo innatarajia kunufaisha wakulima 30,000 wa mikoa hiyo.
“Kampuni imefanikiwa kununua kiwanda hiki na kufanya makubaliano na Benki ya Mendeleo ya Kilimo (TADB), Vyama vya Wakulima (AMCOS) kama suluhisho la uhakika wa soko la mazao ya wakulima ambapo kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 100 za unga kwa siku” alisema Balukuli.
Katika hatua nyingine Balukuli alisema tayari wamepata soko la unga na mahindi ambapo mikataba imeingiwa na wafanyabiashara toka Kigali tani 1000 za mahindi, Zambia tani 10,000 za unga , Mombasa Kenya tani 10,000 za mahindi na Lubumbashi Congo tani 10,000 za mahindi pia kampuni ya Double Dream Holding ya Nairobi Kenya inahitaji tani 5,000 za mahindi.
Mwekezaji huyo aliomba uongozi wa serikali kusaidia kutoa elimu kwa wakulima juu ya ubora wa mahindi ili kuwa na uhakika wa bidhaaa zitakazozalishwa pia kanuni bora za kilimo ili kuepuka tatizo la sumukuvu kwenye mazao.
“Tuna changamoto ya mahindi machafu kutokana wakulima kutokuwa na elimu. Tunaomba mkoa utusaidie tupate eneo ili tufungue shamba darasa la kufundisha wakulima kuanzia matumizi ya mbegu bora, pembejeo hadi uvunaji sahihi (post-harvest). Sisi tutafadhili shamba hilo na kutoa wataalam wetu wa kilimo” alisema Balukuli.
Diwani wa Kata ya Malangali Mary Kipalasha alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti kwa jitihada zake zilizosaidia mgogoro wa kiwanda na Tanesco kumalizika na sasa kiwanda kimeanza tena kufanya kazi .
Katika msimu wa kilimo 2020/21 mkoa wa Rukwa ulilenga kuzalisha tani 750,000 za mahindi ambapo uzalishaji uliofikiwa ulikuwa tani 651,433, kati ya hizo mahitaji ya mahindi katika mkoa ni tani 297,315 hivyo kuwa na ziada ya tani 354,117 zinazohitaji soko.
Mwisho.
Imeandaliwa na:
Afisa Habari Mkuu,
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa,
SUMBAWANGA
09.09.2021