Home BUSINESS WAZIRI MKUU ATANGAZA ZABIBU KUINGIZWA KWENYE MAZAO YA KIMKAKATI

WAZIRI MKUU ATANGAZA ZABIBU KUINGIZWA KWENYE MAZAO YA KIMKAKATI

 

DODOMA.

Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim  Majaliwa amesema zao la zabibu litajumuishwa katika mazao ya kimkakati ikiwa ni mkakati wa serikali kuinua zao hilo linalolimwa jijini Dodoma.

Kutokana na hatua hiyo, zabibu zitajumuishwa katika mazao makuu ya kimkakati nchini ambayo ni pamba, kahawa, chai na korosho.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo juzi Ijumaa Agosti 13,katika  ziara yake fupi ya kutembelea mashamba ya wakulima na kiwanda kidogo cha kusindika mvinyo cha Ushirika wa Wakulima wa Zabibu (UWAZAMAM), katika kata ya Matumbulu jijini humo.

Akizungumza na wakulima hao, Waziri Mkuu Majaliwa amewahakikishia mpango wa serikali kuliinua zao la zabibu ikijumuisha uboreshaji wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari Makutupora) kuongeza maofisa ugani waliojengewa uwezo zaidi, utafiti wa mbegu bora na kutafuta uhakika wa masoko ya zabibu ili kumnufaisha mkulima.

“Serikali itahakikisha zao la zabibu linaleta tija kwa mkulima wa Dodoma kwa kuliwekea miundombinu mbalimbali na hivyo kusaidia kukua kwake tumewaomba  TARI kuzalisha miche yenye ubora na ya aina mbalimbali ya zabibu ikiwemo zabibu za mezani ili Watanzania waache kutumia zabibu  zinazoingizwa nchini kutoka nje ya nchi zilizojaa katika maduka na masoko mengi makubwa. 

“Kwa hivi sasa hili zao ni la kimkakati na lengo letu kuu ni kuongeza uzalishaji na kulima kwa tija ili tuiingize Tanzania kwenye ramani ya dunia ya wazalishaji wa zabibu bora na zenye kiwango,” amsema Waziri Mkuu Majaliwa.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe aliwahakikishia wakulima hao dhamira ya serikali katika kukiinua kilimo cha zao la zabibu huku akibainisha moja kati ya mkakati uliopo wa kuongeza kodi katika mvinyo unaoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mheshimiwa Anthony Mavunde, ameishukuru serikali kwa namna inavyolipa kipaumbele kilimo cha zabibu jambo ambalo litaongeza ari kwa wakulima kuzalisha zaidi na kwa tija. 

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuziomba Taasisi za Fedha kusaidia kuwawezesha mitaji ya ununuzi wa mashine za kuchakata zabibu ili wakulima hao kuongeza thamani ya zao la zabibu kwa kuacha kuuza zabibu kama tunda na badala yake kuuza mchuzi wa zabibu ambao una faida zaidi kwa mkulima.

Previous articleMHANDISI NA AFISA MANUNUZI WA HALMASHAURI YA BUNDA, MIKONONI MWA TAKUKURU
Next articleKUTOKA MEZA YA MAGAZETI J.MATATU YA LEO AGOSTI 16-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here