Home BUSINESS WAZIRI BITEKO: MADINI NI RASILIMALI YA TAIFA

WAZIRI BITEKO: MADINI NI RASILIMALI YA TAIFA

  



 
Na: Tito Mselem, Ruvuma

Imeelezwa kuwa, Madini yote ni Rasilimali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yamewekwa chini ya uangalizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya watanzania wote.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko alipotembelea mgodi wa Lutarasi unaochimba madini ya dhahabu uliopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika mkutano na wachimbaji wadogo, Waziri Biteko amewataka wafanyakazi wote wanaofanya kazi katika mgodi huo kuwa waaminifu katika kazi zao na pia amemtaka mmilki wa mgodi huo Johnson Nchimbi kuwatendea haki wafanyakazi wake kwa kuwalipa stahiki zao kwa wakati na kwa kuzingatia makubaliano yao.

Aidha, Waziri Biteko amempongeza Nchimbi kwa kuwekeza fedha nyingi katika mradi wa uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu katika mgodi huo.

“Kuna watu wanachanganya kati ya Haki Ardhi na Haki Madini hizi ni Haki mbili tofauti na kuna watu wanaamini Haki Ardhi inanguvu zaidi kuliko Haki Madini, hapana Haki zote ni sawa na zinasimamiwa na Serikali unapewa wewe Mtanzania kwa muda mfupi,” amesema Waziri. Biteko.

Pia, Waziri Biteko amesema kuna eneo kubwa kule Dar-Poli Wilaya ya Nyasa ambalo leseni yake imeisha muda wake, ambapo ameilekeza Ofisi ya Madini ya Wilaya ya Nyasa walifute ili Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wapeleke vikundi vya watu wanaotaka kuchimba waombe leseni wachimbe ili walete maendeleo katika Mkoa wa wa Ruvuma.

“Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametuelekeza sisi wasaidizi wake tuje tutatue kero zote zilizopo katika maeneo yenu na tutahakikisha migogoro yote tunaipunguza au tunaimaliza kabisa,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amemuhakikishia muwekezaji wa mgodi wa Lutarasi Johnson Nchimbi kupata msaada wowote atakao hitaji kutoka Serikalini ikiwemo kumuunganisha na mabenki yaliopo nchini ili apate mkopo na kuendeleza mgodi wa Lutarasi ambao utawaletea wananchi wa Ruvuma maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema, Nchimbi ni mchimbaji mdogo rukiki ambaye anahitaji kukua na amemtaka achangie ukuaji wa maendeleo ya eneo la Lutarasi ili iendane na uzalishaji uliopo katika eneo hilo ikiwemo uongezaji wa ajira na maendeleo ya mtu mmoja mmoja.   

Pia, Brigedia Ibuge amempongeza Waziri Biteko kwa kufanya ziara katika mkoa wa Ruvuma ambapo amemuahidi kutelekeza maagizo yote aliyoyatoa mkoani humo.
 
Awali Waziri Biteko alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kupokea taarifa ya mwenendo mzima wa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini katika mkoa wa Ruvuma.

 
Credit – Wizara ya Madini.

Previous articleDC KIGAMBONI MHE.FATMA NYANGASSA AZINDUA VIJANA JOGGING CLUB,KIGAMBONI
Next articleMBUNGE NEEMA LUGANGIRA ATOA NENO KUHUSU WABUNGE NA CHANJO YA COVID19

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here