Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wameingia makubaliano yanayolenga kushirikiana katika shughuli za utafiti kwa wachimbaji wadogo ili kubainisha mashapo yenye rasilimali madini na kuleta tija katika sekta ya uchimbaji mdogo.
Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, leo August 27, 2021 katika Ofisi za GST ambapo kwa Pamoja GST na STAMICO wamefurahia hatua hiyo ya ushirikiano katika utendaji kazi utakaoleta tija kiuchumi katika uchimbaji mdogo.
Sambamba na makubaliano hayo Naibu Waziri amewapongeza viongozi na Menejimenti ya STAMICO na GST kwa kuona Taasisi za serikali zinaanza kufanya kazi kwa kushirikiana jambo litakalo saidia kuondoa mkanganyiko katika kuwahudumia wachimbaji wadogo ambao wanahitaji huduma za utafiti wa madini.
Akizungumzia juu ya kupatikana kwa matokeo chanya ya makubaliano hayo, Prof.Manya amezitaka Taasisi hizi kuongeza bidiii na kufanya tathimini ya utekelezaji wa makubaliano haya ili kudhihirisha umuhimu wa makubaliano haya kwa wachimbaji wadogo nawadau wa madini na Taifa kwa ujumla
Akiongea juu ya majukumu ya STAMICO katika makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amesema kila Taasisi inamajukumu yake ambapo STAMICO ina jukumu la kisheria la kuwaendeleza na kuwalea wachimbaji wadogo wakati GST ina wajibu kufanya utafiti na kubainisha maeneo yenye madini nchi nzima.
Dkt.Mwasse aliendelea kuelezea kuwa makubaliano haya yanaenda kuunganisha nguvu ambapo kwa kutumia wataalamu na vifaa kutoka taasisi hizi mbili , zitaleta tija katika kuwalea wachimbaji wadogo na kuwasaidia kufanya uchimbaji wa uhakika na wenye tija kiuchumi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amesema makubaliano haya yanaenda kuongeza thamani kubwa katika sekta ya uchimbaji mdogo kwa kuwa GST wanatoa taarifa za upatikanaji wa madini wakati STAMICO inavifaa vya kisasa vitakavyosaidia kufanya utafiti wa kina katika maeneo ya wachimbaji wadogo hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya uchimbaji mdogo nchini.
Dkt. Budeba alieleza kuwa taasisi hizi mbili zina wataalamu wa kutosha hivyo zimeona ni vyema kupeleka utalaamu huo kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa wao ndio wawekezaji pekee tutakao baki nao katika kuendeleleza sekta ya madini nchini.