Home BUSINESS STAMICO NA GST WAINGIA MAKUBALIANO YA KUIMARISHA UTAFITI KATIKA UCHIMBAJI MADINI

STAMICO NA GST WAINGIA MAKUBALIANO YA KUIMARISHA UTAFITI KATIKA UCHIMBAJI MADINI

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) wameingia makubaliano yanayolenga kushirikiana katika shughuli za utafiti kwa wachimbaji wadogo ili kubainisha mashapo yenye rasilimali madini na kuleta tija katika sekta ya uchimbaji mdogo.

Makubaliano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, leo August 27, 2021 katika Ofisi za GST ambapo kwa Pamoja GST na STAMICO wamefurahia hatua hiyo ya ushirikiano katika utendaji kazi utakaoleta tija kiuchumi katika uchimbaji mdogo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Madini Prof. Manya amesema makubaliano hayo ni mwanzo mzuri wa kuleta maamuzi ya pamoja yatakayo mrahisishia mchimbaji mdogo kupata matokeo ya kiutafiti wa madini kwa kuwa Taasisi hizi mbili zina majukumu yanayokamilishana katika suala zima la kufanya utafiti na kuleta matokeo chanya kwa wachimbaji.

Sambamba na makubaliano hayo Naibu Waziri amewapongeza viongozi na Menejimenti ya STAMICO na GST kwa kuona Taasisi za serikali zinaanza kufanya kazi kwa kushirikiana jambo litakalo saidia kuondoa mkanganyiko katika kuwahudumia wachimbaji wadogo ambao wanahitaji huduma za utafiti wa madini.

Akizungumzia juu ya kupatikana kwa matokeo chanya ya makubaliano hayo, Prof.Manya amezitaka Taasisi hizi kuongeza bidiii na kufanya tathimini ya utekelezaji wa makubaliano haya ili kudhihirisha umuhimu wa makubaliano haya kwa wachimbaji wadogo nawadau wa madini na Taifa kwa ujumla

“Sisi kama Wizara tunatambua STAMICO ina wajibu wa kuwalea na kuwasimamia wachimbaji wadogo, wakati huo huo GST ndio wanaopaswa kufanya tafiti na hatimae kutoa ramani za wapi viashiria vya uwepo wa madini vilipo;  napenda kuamini kuwa ushirika huu unaoanza kwa kutiliana saini unakwenda kuondoa kabisa tatizo mkanganyiko kwa wachimbaji wadogo juu ya wapi waende kupata taarifa za utafiti wa madini kati ya STAMICO au GST”

Akiongea juu ya majukumu ya STAMICO katika makubaliano hayo Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amesema kila Taasisi  inamajukumu yake ambapo STAMICO ina jukumu la kisheria la kuwaendeleza na kuwalea wachimbaji wadogo  wakati GST ina wajibu kufanya utafiti na kubainisha maeneo yenye madini nchi nzima.

Dkt.Mwasse aliendelea kuelezea kuwa makubaliano haya yanaenda kuunganisha nguvu ambapo kwa kutumia wataalamu na vifaa kutoka taasisi hizi mbili , zitaleta tija katika kuwalea wachimbaji wadogo na kuwasaidia kufanya uchimbaji wa uhakika na wenye tija kiuchumi.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba amesema makubaliano haya yanaenda kuongeza thamani kubwa katika sekta ya uchimbaji mdogo kwa kuwa GST wanatoa taarifa za upatikanaji wa madini wakati STAMICO inavifaa vya kisasa vitakavyosaidia kufanya utafiti wa kina katika maeneo ya wachimbaji wadogo hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya uchimbaji mdogo nchini.

Dkt. Budeba alieleza kuwa taasisi hizi mbili zina wataalamu wa kutosha hivyo zimeona ni vyema kupeleka utalaamu huo kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa wao ndio wawekezaji pekee tutakao baki nao katika kuendeleleza sekta ya madini nchini.

Sambamba na Naibu Waziri wa Madini Prof.  Shukrani Manya wadau wengine waliokuwepo katika makubaliano hayo ni Pamoja na Kamishna wa Madini Mha. David Mlabwa, Madini, Kamishna Msaidizi,Mazingira Zephania Nsungi na wataalam mbalimbali kutoka GST na STAMICO.

Previous articleRC MAKALLA AKERWA NA KASI NDOGO YA MKANDARASI BARABARA YA MAKONGO
Next articleMBUNIFU NEAH ATAMBA KUITEKA MISS TANGA KESHO KWA MAVAZI YAKE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here