Na; Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM.
MASHINDANO ya Miss Afrika kwa mara ya kwanza yanatarajia kufanyika nchini Tanzania Novemba 26,mwaka huu ambapo yanatarajia kushirikisha nchi 16 katika ukanda wa Afrika mashariki.
Akizungumza hayo jana mkoani Dar es Salaam,Rais wa Mashindano hayo,Rena Callist,wakati alipotembelea maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Tantrade akiambatana na Mabalozi wa mbalimbali wa mashindano hayo wakiwemo Mshindi wa Mashindano hayo kwa mwaka juzi wa nchini Rwanda.
Alisema lengo la kutembelea maonesho hayo ni kuangalia fursa mbalimbali
ambazo wanaweza kuzitangaza kupitia mashindano yao ya Miss Afrika ambayo yanaonyeshwa Dunia Nzima.
Alisema takribani nchi 16 ushiriki katika mashindano hayo hivyo ni fursa nzuri kwa nchi ya Tanzania kwa sasa kushiriki katika kuonyesha matangazo yao ambayo yatafanya kupata wawekezaji wakavutika na kuja kuwekeza katika nchi huku bidhaa za nchi zikatangazwa kupitia mashindano hayo.
“Ukizingatia mashindano yetu yanaonyesha live watu zaidi ya milioni 300 wanaangalia kwa hiyo ni fursa nzuri ya watanzania kwa pamoja kujitangaza kupitia mashindano hayo,tumefurahi kuja kutembea katika maonesho ya mwaka huu kwani yamekuwa mazuri,”alisema Callist.
Alisema kupitia mashindano hayo watu wanaweza kuja kujitangaza ili bidhaa za ndani ziweze kujulikana kwa nchi za Afrika mashariki wakazinunua ili kupata soko.
“Kama mnavyofahamu Afrika mashariki ni kubwa hivyo ni fursa nzuri wao kujitangaza …katika kutembea tumevutiwa zaidi ya banda la maliasili hasa katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania,”alisema.