Home LOCAL WANANCHI KATA YA MILO WAOMBA ELIMU YA UWATIKAJI.

WANANCHI KATA YA MILO WAOMBA ELIMU YA UWATIKAJI.

Diwani wa kata ya Milo Robert Njavike akiongea na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa kujadili changamoto na maendeleo ya kata hiyo

Wananchi mbalimbali wa kata ya Milo Wilayani Ludewa wakimsikiliza Diwani wao Robert Njavike kwenye mkutano wa hadhala uliofanyika Juni 2 kwenye Kijiji cha Mapogolo kata ya Milo.
Na: Damian Kunambi, NJOMBE.

Ikiwa zimepita siku chache toka diwani wa kata ya Milo wilayani Ludewa Robert Njavike atoe amri kwa wananchi wake juu ya kulima zao la kimkakati la parachichi miti 10 kwa kila kaya hatimaye wananchi hao waomba kupewa elimu ya uwatikaji miche hiyo.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mapogolo kwenye kata hiyo uliolenga kujadili changamoto na masuala ya maendeleo.

Wananchi hao wamesema kuwa endapo watapatiwa elimu hiyo ya kiwatika miche itakuwa ni jambo rahisi kwao kufanya kilimo hicho kwa urahisi zaidi.

Blantina Mtweve ni miongoni mwa wananchi hao amesema kuwa ili waweze kulima miti mingi ni vyema wakajifunza jinsi ya kuwatika ambapo itawasaidia kupata miti mingi zaidi.

“Agizo hili lililotolewa na diwani wetu tumelipokea vizuri sana kwakuwa ni jambo ambalo limelenga kutunufaisha sisi moja kwa moja hivyo tunaomba tusaidiwe elimu ya uwatikaji ili tuweze kutimiza jambo hili“, Alisema Mtweve.

Aidha diwani huyo amelipokea ombi hilo na kuwaagiza viongozi wa kata kuunda timu ya wataalamu itakayozunguka maeneo yote ya vijiji ili kutoa elimu hiyo.

Amesema kuwa kwakuwa yeye ni kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha wananchi wake wanakua kiuchumi hivyo hiyo ni njia mojawapo ya kukuza uchumi huo.

Amesema endapo wananchi wake watakua kiuchumi itawasaidia kusomesha watoto wao katika mazingira mazuri ikiwemo kupata fedha za kukidhi mahitaji yao.

“Tunapaswa kujikita katika kilimo cha mkakati ili tuweze kuinuka kiuchumi katika familia zetu, kata na wilaya kiujumla“, alisema Njavike.

Nao viongozi hao wa kata wamelipokea vyema suala hilo na kuahidi kuungana na diwani huyo katika kuhamasisha wananchi juu ya kilimo hicho cha parachichi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here