MKUU wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kuepuka migongano na mivutano isiyokuwa na tija ambayo imekuwa chanzo kwa Halmashauri kushindwa kutekeleza mipango yake, na kusababisha wananchi kukosa baadhi ya huduma za kijamii.
Badala yake, amewataka wajikite zaidi kuijenga Halmashauri yao kwa kubuni vyanzo vipya na kuelekeza nguvu kubwa katika kukusanya na kusimamia mapato yanayopatikana ili kuharakisha maendeleo na uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.
Balozi Ibuge, amesema hayo jana wakati akizungumza na madiwani,watumishi na viongozi wa wilaya hiyo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Amesema, katika maisha ya kawaida hakuna binadamu wanaoweza kuishi bila kutofautiana kwa sababu mbalimbali,lakini kwa viongozi waliochaguliwa na walioteuliwa ni muhimu kumaliza tofauti zao kwa maslahi ya wananchi na uhai wa Halmashauri yao.
“Nilipoteuliwa na mwenye dhamana Mheshimiwa Rais Samiha Suluhu Hassan alinipa imani nije kumwakilisha mkoa wa Ruvuma na sijiwakilishi mimi, nataka nisimamie maendeleo kwa kushirikiana na nyinyi”amesema.
Amesema, kutokana na ulezi wake kwenye Halmashauri za wilaya hataki kuona wala kusikia migogoro isiyokuwa na tija kwa madiwani na kuhakikisha wanamaliza tofauti zao,kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja.
Akizungumzia juu ya matokeo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioshia tarehe tarehe 30 Juni 2020 amesema, Halmashauri ya Namtumbo haijafanya vizuri ikilinganishwa na rekodi zinazoonesha kwa miaka minne iliyopita imefanya vizuri tofauti na hesabu za mwaka wa fedha 2019/2020 baada ya kupata hati yenye mashaka.
Amesema, kwa mujibu wa taarifa za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali(CAG)msingi wa kupata hati yenye mashaka ni kutokana na hati za madai zilizoidhinishwa kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato(LGRCIS)bila ya kuwa nyaraka toshelezi ambapo kiasi cha shilingi 191,935,660.00 hazijulikani zilipo.
Amesema, Halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka siyo jambo jema kwakuwa ina eneo kubwa kijiografia,wananchi wanaojituma katika shughuli za uzalishaji na hali ya hewa nzuri.
Amesema, pamoja na kupata hati yenye mashaka, lakini hata mwenendo wa kufanyia kazi taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali bado ni wa kusuasua.
Balozi Ibuge amesema, hali hiyo imejionesha kutokana na utekelezaji wa hoja na mapendekezo yaliyotolewa na CAG ambapo Halmashauri imeweza kufunga hoja 38 kati ya 100 za miaka ya nyuma,hivyo kusalia na hoja 62 kwa taarifa ya hesabu jumuishi.
Amesema, kuwepo kwa hoja nyingi za CAG ambazo bado hazijafungwa na maagizo ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ambayo hayajafanyiwa kazi hadi sasa haitoi picha nzuri na ishara kuwa menejimenti ya Halmashauri haizipi uzito unaostahili katika kujibu na hivyo kukosa majibu yanayotosheleza.
Balozi Ibuge ameagiza uongozi wa Halmashauri kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa kujibu maagizo ya kamati ya kudumu ya Bunge nah ja za ukaguzi ambazo bado hazijafungwa kabla ya tarehe 30 Septemba 2021.
Kwa upande wak mweka hazina wa Halmashauri hiyo Pendo Nyomeye amesema, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kulikuwa na hoja 29,zilizofungwa 14 na 15 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sofia Kizigo amesema,katika wilaya hiyo kuna vyanzo vingi,hata hivyo mapato yanayokusanywa hayalingani na vyanzo vilivyopo kutokana na baadhi yake kutoroshwa kwenda nje ya mfumo na mengine yanaishia kwa wajanja wachache.
Amesema, kupata hati yenye mashaka imeongeza ari ya kujituma na kufanya vizuri zaidi katika suala zima la kukusanya mapato na kuhaidi kufanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
MWISHO.