Home LOCAL MADIWANI NAMTUMBO WAONYWA JUU YA MIGOGORO

MADIWANI NAMTUMBO WAONYWA JUU YA MIGOGORO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya  Namtumbo mkoani Ruvuma Juma Pandu akifungua kikao cha Baraza la madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kujadili na hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambayo Halmashauri hiyo imepata hati yenye mashaka,kulia mkuu wa mkoa huo Balozi Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sofia Kizigo akizungumza jana katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo kilichojadili hoja na kupitia maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ,katikati Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho na wa pili kushoto Mkuu wa mkoa huo Balozi Bigadia Jenerali Wilberti Ibuge,

Na: Muhidin Amri. NAMTUMBO.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Balozi Wilbert Ibuge, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kuepuka migongano na mivutano isiyokuwa na tija  ambayo imekuwa chanzo kwa Halmashauri  kushindwa kutekeleza mipango yake,  na kusababisha wananchi  kukosa  baadhi ya huduma za kijamii.

Badala yake,  amewataka wajikite zaidi  kuijenga Halmashauri yao kwa kubuni vyanzo vipya na kuelekeza nguvu kubwa katika kukusanya na kusimamia mapato yanayopatikana ili kuharakisha maendeleo na uchumi wa wananchi wa wilaya hiyo.

Balozi  Ibuge, amesema hayo jana wakati akizungumza na madiwani,watumishi na viongozi wa wilaya hiyo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa ya mdhibiti na mkaguzi  mkuu wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema, katika maisha ya kawaida hakuna binadamu wanaoweza kuishi bila kutofautiana kwa sababu mbalimbali,lakini kwa viongozi waliochaguliwa na walioteuliwa ni muhimu kumaliza tofauti  zao kwa maslahi ya wananchi na uhai wa Halmashauri yao.

“Nilipoteuliwa na mwenye dhamana Mheshimiwa Rais Samiha Suluhu Hassan alinipa imani nije kumwakilisha  mkoa wa Ruvuma na sijiwakilishi mimi, nataka nisimamie maendeleo kwa kushirikiana na nyinyi”
amesema.

Amesema, kutokana na ulezi wake kwenye Halmashauri za wilaya hataki kuona wala kusikia migogoro isiyokuwa na tija  kwa madiwani na  kuhakikisha wanamaliza tofauti zao,kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumzia juu ya matokeo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioshia tarehe tarehe 30 Juni 2020 amesema, Halmashauri ya Namtumbo haijafanya vizuri ikilinganishwa na rekodi  zinazoonesha kwa miaka minne iliyopita imefanya vizuri tofauti na hesabu za mwaka  wa fedha 2019/2020 baada ya kupata hati yenye mashaka.

Amesema, kwa mujibu wa taarifa za mkaguzi na mdhibiti  wa hesabu za Serikali(CAG)msingi wa kupata hati yenye mashaka ni kutokana na hati za madai zilizoidhinishwa kwenye mfumo wa ukusanyaji mapato(LGRCIS)bila ya kuwa nyaraka toshelezi ambapo kiasi cha shilingi 191,935,660.00 hazijulikani zilipo.

Amesema, Halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka siyo jambo jema kwakuwa ina eneo kubwa kijiografia,wananchi wanaojituma katika shughuli za uzalishaji na hali ya hewa nzuri.

Amesema, pamoja na kupata hati yenye mashaka, lakini hata  mwenendo wa kufanyia kazi taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za Serikali bado ni wa kusuasua.

Balozi Ibuge amesema, hali hiyo imejionesha kutokana na utekelezaji wa hoja na mapendekezo yaliyotolewa na CAG ambapo Halmashauri imeweza kufunga hoja 38 kati ya 100 za miaka ya nyuma,hivyo kusalia na hoja 62 kwa taarifa ya hesabu jumuishi.

Amesema, kuwepo kwa hoja nyingi  za CAG ambazo bado hazijafungwa na maagizo ya kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa ambayo hayajafanyiwa kazi hadi sasa haitoi picha nzuri  na ishara kuwa menejimenti ya Halmashauri haizipi uzito unaostahili katika kujibu na hivyo kukosa majibu yanayotosheleza.

Balozi Ibuge ameagiza uongozi wa Halmashauri kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa kujibu maagizo ya kamati ya kudumu ya Bunge nah ja za ukaguzi ambazo bado hazijafungwa kabla ya tarehe 30 Septemba 2021.

Kwa upande wak mweka  hazina wa Halmashauri hiyo Pendo Nyomeye amesema, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 kulikuwa na hoja 29,zilizofungwa 14 na 15 ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sofia Kizigo amesema,katika wilaya hiyo kuna  vyanzo vingi,hata hivyo mapato yanayokusanywa hayalingani na vyanzo vilivyopo kutokana na baadhi yake kutoroshwa kwenda nje ya mfumo na mengine yanaishia kwa wajanja wachache.

Amesema, kupata hati yenye mashaka imeongeza ari ya kujituma na kufanya vizuri zaidi katika suala zima la kukusanya mapato na kuhaidi kufanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
MWISHO.


Previous articleTIMU YA YANGA YAILAZA RUVU SHOOTING 3-2 DIMBA LA MKAPA.
Next articleMTENDAJI KATA YA CHELA AWAPONGEZA WACHIMBAJI WADOGO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here