Na: Muhidin Amri, MBINGA
Halmshauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,katika kipindi cha miaka miwili imetoa shilingi 344,049,155.07 kwa vikundi 17 vya vijana,wanawake na walemavu ili kuvijengea uwezo kiuchumi.
Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri hiyo Pascal Ndunguru amesema hayo jana wakati wa kukabidhi kiwanda cha kufyatua tofali kwa kikundi cha vijana cha Chipukizi Kigonsera ikiwa ni Utekelezaji wa sheria na maagizo ya serikali ya kutenga asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kwa mujibu wa Ndunguru, tangu mpango huo ulipoanza kutekelezwa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga imeshatoa zaidi ya shilingi 560,000,000 ambazo zimekwenda kwenye vikundi mbalimbali na kwa wananchi.
Alisema,pamoja na kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kukopesha asilimia kumi,Halmashauri ya wilaya Mbinga iliamua kujielekeza zaidi katika falsafa ya kukopesha mitaji na vitendea kazi kwa lengo la ukuzaji na uendelezaji wa viwanda.
Ndunguru alisema, kiwanda hicho kina seti moja ya mashine ya kuchanganya zege,mashine ya kuchanganya mchanganyiko wa mchanga na saruji vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 17,549,999.07.
Alisema, kiwanda hicho cha vijana kina uwezo wa kufyatua tofali za kisasa,ngumu na zenye ubora unaokidhi mahitaji ya majenzi ya Serikali na kwa siku kina uwezo wa kufyatua tofali 2000 na vijana hao wamepatiwa mafunzo ya kuendesha mitambo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Juma Mnwele alisema pamoja na seti ya mashine,Halmashauri imetoa shilingi milioni 4,680,000 kwa kikundi hicho kama mtaji na hivyo kufanya mkopo wote kufikia shilingi milioni 22,229,999.
Alisema, kwa kuanzia kiwanda kitaanza kufyatua tofali kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya kwa makubaliano ya kufyatua tofali 28,000 na hivyo kujipatia kipato moja kwa moja.
Aidha alisema, mtambo wa kukoroga zege utakodishwa na Halmashauri kwa makubaliano ya ujirani mwema kwa pande zote mbili na vijana hao wataendelea kupata kazi nyingi za serikali na watu binafsi ikiwemo tofali kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya.
Mwenyekiti wa kikundi Kenneth Mbena alisema,kikundi kilifikia uamuzi wa kuomba mkopo wa mashine ya kufyatua tofali hasa baada ya kuona kuna fursa ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri pamoja na jengo la Utawala.
Hata hivyo alisema, matumaini yao kuendelea kupata kazi hata baada ya miradi hiyo miwili kukamilika kwani wamejipanga kuhakikisha wanazalisha tofali bora zitakazotumika kwenye miradi ya ujenzi.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Mbinga kwa kutoa fedha za kujenga kiwanda hicho ambacho kitasaidia wananchi kupata tofali bora kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi na ofisi za serikali.
Alisema, kuanzishwa kwa kiwanda hicho kinakwenda kufungua fursa mpya kwa wakazi wa Mbinga kuanza kujenga nyumba kwa kutumia tofali za saruji na mchanga badala ya mazoea ya kujenga kwa kutumia tofali za udongo.
Amewaasa wana kikundi hicho kuhakikisha wanazalisha tofali zenye ubora ili waweze kujitangaza na kupata soko kubwa la ndani nan je ya wilaya ya Mbinga.
MWISH