Home LOCAL DKT, OGUNDE ATOA WITO WATANZANIA KUENDELEZA UTALII, UFAFANUZI WATOLEWA USALAMA MAPANGO YA...

DKT, OGUNDE ATOA WITO WATANZANIA KUENDELEZA UTALII, UFAFANUZI WATOLEWA USALAMA MAPANGO YA AMBONI TANGA.

Na: Maiko Luoga TANGA. 

Watanzania wameaswa kuyalinda na kuendeleza maeneo ya utalii yaliyopo katika maeneo tofauti nchini ambayo ni tunu pekee Taifa limebarikiwa kuwa nayo na hayawezi kupatikana maeneo mengine Duniani zaidi ya Tanzania.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Canon, Dkt, Mecka Ogunde juni 21/2021 alipotembelea vivutio vya utalii vya mapango ya Amboni Mkoani Tanga na kujionea mazingira bora ya uhifadhi yaliyotunzwa na kuendelezwa na Serikali.

“Nimepata fursa ya kutembelea maeneo haya ya vivutio vya kihistoria katika mapango ya Amboni Tanga hakika tumeshuhudia kuona uwezo na ukuu wa Mungu katika eneo hili maana tumeona mambo mengi makubwa ndani ya mapango haya ambayo tunaambiwa yapo hapa kwa zaidi ya miaka milioni 150 iliyopita” Dkt, Mecka Ogunde.

Aidha Dkt, Ogunde Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania amesema kila Mtanzania analo jukumu kubwa la kulinda na kuvitunza vivutio hivyo pamoja na kuvitangaza ndani na nje ya Tanzania ili vipate watalii wengi ambao watatembelea na kuongeza uchumi wa Taifa.

“Tumejaliwa kuwa na maeneo mengi yenye utalii mkubwa katika nchi yetu, tunao wajibu wa kutangaza maeneo haya ndani na nje ya ili Mataifa yatambue mambo haya tuliyozawadiwa na Mwenyezi Mungu nao wakifika hapa watasaidia kukuza pato la Taifa letu” Dkt, Mecka Ogunde Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania.

Bw, Emmanuel Daniel mwongoza watalii katika hifadhi ya Mapango ya Amboni Mkoani Tanga amesema safari ya Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana katika maeneo hayo ni mafanikio makubwa kwao kwakuwa inaimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa hilo ambalo lina nafasi kubwa ya kuijulisha Jamii uwepo wa hifadhi hiyo na kuitembelea.

“Tunashukuru ujio wa Katibu Mkuu wa Kanisa Anglikana katika eneo hili la mapango ya Amboni tunaamini Kanisa hili litasaidia kuwajulisha Waumini wake na Jamii kwa ujumla uwepo wa mapango haya ili waweze kuyatembelea na kujifunza mambo mengi mazuri yaliyopo hapa” alisema Emmanuel Daniel.

Hatahivyo alitumia nafasi hiyo kuwaondoa hofu Watanzania ambao wamekuwa wakifikiri kuwa mapango hayo yalivamiwa na wahalifu waliokuwa wakitisha usalama katika maeneo ya Mkoa wa Tanga na kusema kuwa eneo hilo ni salama halijawahi kuvamiwa na wahalifu wowote tofauti na taarifa zilivyokuwa zikiripotiwa hapo awali.

“Baadhi ya vyombo vya Habari vilikuwa vikiripoti tofauti kuwa mapango haya yalitumiwa na wahalifu jambo hili si kweli maana wahalifu hao walijificha kwenye mapango mengine yaliyopo kwenye Kijiji cha Mabatini huko mpakani Horohoro ndipo walipojificha sio hapa Amboni”

Amesema mkanganyiko huo wa Taarifa uliathiri shughuli za utalii katika Mapango ya Amboni kwakuwa watu wengi waliingia hofu ya uwepo wa matukio ya kihalifu katika eneo hilo na kushindwa kutembelea kwakuhofu usalama, huku akisisitiza kuwa mapango hayo yapo salama chini ya usimamizi wa Serikali.

“Tulipitia kipindi kigumu kwakuwa watalii wengi walikuwa wanashindwa kufika hapa wakihofu usalama wao, jina Hamboni lilikuwa linatumika sana kwenye matukio ya Habari kueleza kuwa wahalifu hao walijificha kwenye mapango ya Amboni jambo ambalo si kweli tunawaeleza kuwa tupo salama” alieleza Emmanuel Daniel.
Previous articleBRELA YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUFANYA USAFI, KUWAFARIJI WAGONJWA NA KUCHANGIA DAMU NA KUTOA ELIMU
Next articleKARIBU USOME MAGAZETI YA LEO ALHAMISI JUNI-24-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here