Home BUSINESS BRELA YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUFANYA USAFI, KUWAFARIJI WAGONJWA...

BRELA YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUFANYA USAFI, KUWAFARIJI WAGONJWA NA KUCHANGIA DAMU NA KUTOA ELIMU

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bi. Roida Andusamile akitoa maelezo kuhusu misaada mbalimbali iliyotolewa na BRELA katika hospitali ya Amana Juni 23, 2021, ikiwa ni sehemu ya hitimisho la maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2021 hadi Juni 23, 2021.

Watumishi kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wakifanya usafi katika soko la Kisutu jijini Dar es Salaam leo Juni 23, 2021 ikiwa ni hitimisho la maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza  Juni 16,2021 hadi Juni 23, 2021. 

Watumishi wa BRELA wakiwa katika picha ya pamoja na Afisa Masoko Msaidizi wa Soko la Kisutu Bw. Titus Telesphory (katikati) mara baada ya kufika katika soko hilo, kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya usafi Juni 23, 2021, ikiwa ni sehemu ya hitimisho la Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2021 hadi Juni 23, 2021.  

Na: Mwandishi Wetu,

Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA) imeadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea wagonjwa  katika hospitali ya Amana, kufanya usafi na kuwapatia elimu  juu ya huduma za usajili wa Biashara na Lesini kwa wafanyabiashara katika soko la Kisutu, jijini Dar es Salaam.

 Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ilianza Juni 16 na  kilele chake kufikia  Juni 23. Ambapo Wizara na  taasisi zake zinatakiwa kutoa huduma kwa wadau wake na wananchi kwa ujumla kutokana na michango wanayoitoa kwa serikali yao. 

Wakiwa katika hospitali ya Amana, Watumishi  wa  BRELA walikabidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa ikiwa ni pamoja na Sabuni, Taulo za Kike (Pads) na Daipers za watoto na wakubwa.  Pia walitumia fursa hiyo kuchangia damu. 

Mkuu wa Kitengo cha Uhusuano kutoka BRELA  Bi. Roida Andusamile akizungumza wakati wa kukabidhi bidhaa hizo alisema taasisi hiyo pamoja wa kuwezesha biashara kwa kusajili Majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, utoaji wa Leseni za Biashara kundi A na Leseni za Viwanda na Hataza,  inajali jamii inayoizunguka  kwa kuwapatia msaada pindi fursa inapopatikana. 

“BRELA imefika hospitali ya Amana na kuchangia mahitaji ya msingi ya wazazi na watoto ili wanapoendelea na matibabu wawe katika hali ya usafi,” alifafanua Bi. Andusamile na kuongeza kuwa utaratibu huu utaendelea kufanyika katika hospitali mbalimbali za hapa nchini.

Akipokea msaada huo, Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinamama Dkt. Baya Kissiwa ameishukuru BRELA kwa  msaada iliyo utoa kwa wagonjwa  na kutoa wito kwa taasisi zingine kufika hospitalini hapo na kuwasaidia wagonjwa .

Dkt. Bingwa alisema kuwa hospitali hiyo kwa sasa ina uhitaji mkubwa wa damu  hasa kwa wazazi wanaofika hospitalini hapo kwa matibabu, hivyo inawaomba wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Aidha katika soko la Kisutu, watumishi wa BRELA walitoa elimu kwa wafanyabiashara na kuwahimiza kufanya sajili za biashara ili kuzipa utu wa kisheria biashara zao.  Pamoja na kutoa elimu sokoni hapo, Watumishi wa BRELA walifanya usafi ndani ya soko hilo, ikiwa ni moja ya jukumu la watumishi wa umma kuwajibika kwa wananchi. 

Awali Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Seka Kasela alitumia Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuwahudumia wateja waliofika katika ofisi za BRELA kupata huduma mbalimbali. 

Maadhimisho haya yanaoyoratibiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora yalifanyika sambamba na kaulimbiu “Kujenga Afrika tunayoitaka, kupitia utamaduni wa uadilifu ambao unastawisha uongozi wenye maono hata katika mazingira ya mgogoro.”  

 MWISHO




Previous articleTANZANIA NA POLAND ZAKUBALIANA KUIMARISHA HUDUMA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA KWENYE MAJIJI YA DODOMA NA DAR ES SALAAM
Next articleDKT, OGUNDE ATOA WITO WATANZANIA KUENDELEZA UTALII, UFAFANUZI WATOLEWA USALAMA MAPANGO YA AMBONI TANGA.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here