Home LOCAL DKT. KABATI AIPA SERIKALI MKAKATI WA KUBORESHA SEKTA YA UTALII NA MALIASILI...

DKT. KABATI AIPA SERIKALI MKAKATI WA KUBORESHA SEKTA YA UTALII NA MALIASILI NCHIHI.


DODOMA

Serikali imeshauriwa kuongeza kasi na kukamilisha haraka mradi wa kukuza utalii nyanda za juu Kusini (REGROW) ili kusaidia sekta ya utalii katika mikoa ya nyanda za juu kusini kuweza kushindana na mikoa ya kaskazini.

Akichangia katika hotuba ya wizara ya Maliasili na Utalii, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa, (CCM) amesema wananchi wa mikoa ya nyada za juu Kusini wanategemea mradi wa REGROW kukamilika pindi ifikapo mwaka 2023 kutokana na umuhimu wake katika sekta ya Utalii kusini.

Dkt. Kabati amesema mradi huu utasaidia ongezeko la ajira nyanda za juu kusini pamoja na kuongeza pato katika mikoa hiyo kutokana na kujengwa kwa makao makuu ya mradi Iringa na vyuo vingi vya misitu, na vya utalii. 

Aidha, Kabati ameshauri kuwepo kwa mashindano maalum kwa watendaji wa maliasili na Utalii kutoka kanda ya kusini na kaskazini kuhusu masuala ya Utalii ili kuongeza ufanisi katika sekta ya maliasili na utalii.

“Na ikiwezekana kuwepo na mashindano kati ya kanda ya kusini na kaskazini ili kuongeza ufanisi kwa watendaji wa sekta wa Utalii wa kanda hizi”

Katika hatua nyingine Dkt. Kabati ameitaka serikali kujikita katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii na kuhamasisha zaidi watalii wa ndani kutokana na kuwepo kwa vivutio vingi nchini ambavyo bado havijatangazwa ipasavyo kuongeza utalii wa ndani.

“kwa hiyo niombe matangazo yaongezeke kwa kuwa biashara ni matangazo tukitangaza vizuri hata watalii wa ndani wataongezeka”

Pia katika mchango wake, Kabati ameiataka serikali kuboresha barabara inayoelekea mbuga ya Taifa ya Wanyama ya Ruaha iliyopo mkoani Iringa kutokana na changamoto ya barabara inayoweza kukwamisha ongezeko la watalii mbugani.

“Hii mbuga ni ya pili kwa ukubwa lakini imesahaulika barabara haipitiki kabisa, kwa hiyo niombe mawaziri wote watoe kipaumbele kwa hii barabara ili kukuza utalii wa mbuga hii”

Kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo Iringa, Dkt. Kabati amesema serikali inapaswa kukumbuka vivutio vyote pamoja na kuviwekea mkakati wa kuboreshwa na kutangazwa ikiwepo eneo walipokuwa wakinyongwa wapiganaji na askari wa Kihehe, lililopo Kitanzani, Iringa Mjini pamoja jiwe linaloongea Gangilonga. Kwa sasa pamesahaulika kabisa.

Katika hatua nyingine, Kabati amesema changamoto kubwa inayotatiza halmashauri nyingi nchini hususani katika sekta ya Utalii ni ukosefu wa maafisa utalii waliowezeshwa kufanya kazi hiyo ya kuboresha mazingira ya utalii katika halmashauri zetu.

“Tatizo kubwa hatuna maafisa utalii katika halmashauri zetu na ndiyo maana tunavivutio vingi kwenye halmashauri lakini havijulikani. sasa serikali ikiwezekana itenge ruzuku au kuwe na kurugenzi kabisa itakayojikita na mambo ya utalii”

Kabati ameitaka serikali kupunguza tozo nyingi katika mazao ya maliasali zinazomkandamiza mwananchi ambaye ndiyo mtumiaji wa maliasili na badala yake kuangalia namna ya kuzipunguza na kuboresha mazingira ya kibiashara katika maliasili.

Mwisho, Dkt. Kabati ameipongeza klabu ya Simba na wizara ya maliasili na Utalii kwa namna walivyoingia makubaliano ya kuitangaza nchi kwa klabu ya Simba kuvaa jezi zilizoandikwa neno la kuhamasisha wageni wengi kutembelea nchini kwetu yaani “Visit Tanzania” pamoja na kuweka picha ya mlima wa Kilimanjaro katika jezi hizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here