DODOMA.
Serikali imeahidi kuijenga barabara ya kutoka Kibaoni hadi Mlowa yenye jumla ya Kilomita 363 ambayo inaunganisha mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe mara baada ya Kilomita zilizobakia kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa Kina kuweza kumalizika.
Hayo yamesemwa na naibu waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Msongwe Kasekenya wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum mkoa wa Rukwa (CCM), Bupe Mwakang’ata, lililohoji ni lini ujenzi wa barabara ya kiwango cha Lami kutoka Kibaoni – Kasansa – Muze – Ilemba – Kilyamatundu – Kamsamba hadi Mlowo utakwenda kuanza kutokana na umuhimu wake.
Katika hatua nyingine naibu waziri, Mhandisi Kasekenya amesema kutokana na barabara hiyo kupita katika eneo la kilimo na hivyo kuwa muhimu kiuchumi serikali imeweza kujenga daraja la Momba lililokuwa kikwazo kwa mawasiliano ya barabara ya mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.
Pia serikali imeshaikarabati barabara hiyo angalau kwa kiwango cha changarawe na hivyo kuifanya iweze kupitika katika vipindi vyote wakati ikisubiri kukamilishwa kwa usanifu wa kina katika maeneo yaliyobaki na hatimae ujenzi wa kiwango cha Lami.
Kwa upande wake, Mbunge Bupe Mwakang’ata ameomba serikali ieleze muda wa uhakika ambapo ujenzi wa barabara hiyo ya Kibaoni hadi Mlowa utaanza ili kurahisisha usafiri katika mikoa hii yenye shughuli ya Kilimo.
Katika Hatua nyingine Bupe Mwakang’ata ameipongeza serikali kwa hatua yake ya kujenga daraja la Momba ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa cha mawasiliano lililogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 17 na hivyo kusaidia wananchi.