Home LOCAL “MAKATIBU WA AFYA KASIMAMIENI NYENZO ZA KAZI NA RASILIMALI: DKT. GWAJIMA

“MAKATIBU WA AFYA KASIMAMIENI NYENZO ZA KAZI NA RASILIMALI: DKT. GWAJIMA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima akiongea na makatibu wa Afya nchini (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Chama Cha Makatibu wa Afya Tanzani(AHSATA) unaofanyika mkoani Morogoro.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya Mvomero Mh.Albinus Mugonya akitoa salamu za Mkoa Kwenye mkutano huo.

Baadhi ya makatibu wa Afya nchini wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Afya ,ambapo walitakiwa   kuwajibika na kusimania maslahi ya watumishi wengine.

Rais wa AHSATA Bw.Daniel Muhochi akiongea wakati wa mkutano huo.Muhochi alisema Katika kikao hicho wamekumbushana  usimamizi na uendeshaji Taasisi zao kwa kuzingatia majukumu yao.

Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Hospitali za Rufaa ya Mikoa kutoka Wizara ya Afya Bw.Daniel Temba akiongea Kwenye kikao hicho.

Picha ya pamoja ya Waziri wa Afya Dkt Dorothy Gwajima na baadhi ya Makatibu wa Afya kutoka Mikoa,Wilaya,Halmashauri,Wizara na Taasisi mbalimbali nchini.

Na. Catherine Sungura, MOROGORO.

Makatibu wa afya nchini wametakiwa kusimamia nyenzo na rasilimali za kuendeshea huduma za afya  zilizopo kwenye maeneo yao ya kazi  kama ilivyo kwenye majukumu yao kwani wao ni kioo na alama ya uendeshaji wa taasisi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa Chama Cha  Makatibu wa Afya Tanzania ( AHSATA) unaofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Gwajima amesema Makatibu wa afya lazima waelewe vizuri majukumu yao  ili kuweza kusimamia na kuendesha taasisi zao vizuri na hatimaye kupata mafanikio kwani  wao ndio watendaji wakuu katika kusimamia mifumo ya afya .

“Tunataka mifumo imara ya afya na kuthamini jinsi Serikali ilivyowekeza kwenye mifumo hii ya afya” alisisitiza Dkt. Gwajima.

“Hata hivyo aliwataka makatibu hao kwenda kuisimamia kauli mbiu yao ya mwaka huu ambayo inasema, “Uimarishaji wa mifumo ya afya ni nguzo muhimu katika usimamizi wa rasilimali za sekta ya afya nchini” kuwa kutokana na kauli mbiu hiyo wanapaswa kuwajibika na kujiongezea thamani ya kazi zao wao wenyewe na kuweza kusimamia  maslahi ya watumishi walio chini yao.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema anatambua kada hiyo ndio pekee haina kurugenzi wizarani, hivyo kuagiza hilo lifanyiwe kazi ya uchambuzi kuona kuna kipingamizi gani kinachozuia hilo iwapo ni jambo lenye tija?

’Lazima tubadilike na tuondoe dhana ya uongozi kwenye afya lazima mtu  awe kada ya utabibu ‘Medical Doctor andaeni kongamano litakalojadili hili,kwani mimi nilipokuwa DMO hata RMO  nilifanikiwa kwa kusaidiwa na kada zingine,hivyo Muuguzi au taaluma nyingine ya afya  anaweza kuongoza taasisi ya afya maana huo ni uongozi na siyo kazi ya taaluma maalumu’

Aliongeza kuwa taasisi itakua na mafanikio endapo katibu wa afya atakua imara na taasisi haitofanikiwa endapo katibu wa afya atakua legelege hivyo lazima kada hiyo isimamie majukumu na kujiamini ili kuweza kuzifanya taasisi kuwa imara.

Pia Dkt. Gwajima amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwapatia fursa na uhuru wenye kuzingatia sheria makatibu wa afya ili kuweza kutekeleza majukumu yao.

Upande wa nidhamu, Waziri huyo aliwataka wanaporudi kwenye vituo vyao wakasimamie nidhamu kwani haitapendeza kuona taasisi wanazozisimamia zinafeli wakati wao ni watendaji wakuu ndani ya sekta ya afya.

Suala la Dawa na kadi za kliniki, Waziri huyo amesema anaona bado Kuna  makosa yanaendelea kutokea licha ya kutoa tamko kwa  baadhi ya vituo vya afya kuacha kuuza kadi hizo hivyo amewataka wasimamie hilo. 

Awali akimkaribisha Waziri wa afya, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya  Mvomero Mh. Albinus Mugonya amewataka makatibu hao kuzingatia  miongozo iliyopo  katika utoaji wa huduma za afya zinazostahili  na kufanya kazi  kwa weledi, uaminifu  na ubunifu  hivyo kutoa huduma bila upendeleo  na kuwajibika kwa umma na kwa kuzingatia miiko na maadili ya taalumma zao.

Naye, Rais wa AHSATA Daniel Muhochi amesema katika mkutano huo watajadili na kubadilishana uzoefu na changamoto wanazokabiliana nazo  na kutoka na njia ni namna gani wanaweza kuzitatua.

Muhochi aliomba ridhaa kwa wizara ili kada hiyo kuwa na baraza la taaluma litakalokuwa linashughulikia maadili  kuweza kuboresha huduma za afya sehemu zao za kazi.

Mwisho

Previous articleMAGAZETI YA LEO ALHAMISI JUNI 17-2021
Next articleBARABARA YA KIBAONI HADI MLOWO KUTENGENEZWA KWA KIWANGO CHA LAMI, WAZIRI AELEZA UMUHIMU WAKE KWA UCHUMI WA RUKWA, SONGWE NA KATAVI

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here