Home LOCAL WATU WENYE MATATIZO YA UGUMBA WAIOMBA JAMII ISIWATENGE.

WATU WENYE MATATIZO YA UGUMBA WAIOMBA JAMII ISIWATENGE.

Picha ya Maktaba.

Na: Mwandishi Wetu, Mtimbira.

HOTUBA iliyosomwa na jamii ya watu wenye matatizo ya ugumba katika Kata ya Mtimbira wilayani Malinyi,Mkoa wa Morogoro  imemtoa  machozi Diwani wa Kata hiyo Jane Komba pale walipomweleza namna jamii hiyo inavyonyasisika na kutengwa.

Mbele ya Diwani huyo ambaye alimuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya kuielimisha jamii namna inavyopaswa kuishi na jamii hiyo ya wagumba na kuitaka iwathamini na kuwatambua kuwa ni miongoni mwa wanajamii na wanahaki zote.

Taarifa hiyo  ambayo iliwasilishwa kwa Diwani Jane ilisema kwamba, kuna familia ambazo zimekuwa zikinyanyapaliwa, na kuwafananisha wao na mapipa ya taka kwa kuwa hawana uwezo wa kuzaa hali ambayo inawapelekea kujiona kana kwamba hawana msaada wowote kwa taifa wakati wapo kwenye orodha ya walipa kodi.

Risala hiyo iliendelea kusema, mbali na unyanyapaaji huo, bado jamii hiyo imekuwa ikiteswa na ndugu wa waume zao na wakati mwingine hutumuliwa na kuondoka bila kutoka na kitu chochote licha ya kwamba wamechuma mali pamoja.

Mmoja wa washiriki na Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania, Shamillah Mohamed Makwenjula,akizungumza katika semina hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki Wilayani humo  alisema jamii hiyo imenyanyisika vya kutosha na hata  yeye mwenyewe amekumbana na kadhia hiyo.

“Nilishawahi kufukuzwa kama  mnyama bila kuondoka na chochote licha ya kuwepo kwa baaadhi ya vitu mbavyo tulitafuta pamoja .” amesema Shamilla

Amevitaka  vyombo vinavyohusika wakiwemo watu wa maendeleo ya jamii na vyombo vya dola kuhakikisha wanasimamia na kukomesha unyanyapaaji na unyanyaswaji huo dhidi yao unaotokana na jamii ambayo haithamini wala kutokuwaheshimu wagumba.

Shamillah amesema Wagumba sio kwamba wao waliutaka  ugumba, bali ni maradhi kama yalivyo maradhi mengine ambayo Mungu Mwenyewe ndio anapanga.

Amesema, yeye alifanikiwa kuishi na mume wake zaidi ya miaka 15 lakini hakubahatika kupata mtoto hali ambayo baadaye ilimletea shida kubwa na kupelekea kipigo kikali ambacho kilimsababishia kupata matatizo katika mfuko wa uzazi.

Zuhura Salum Likwale yeye amesema pamoja na kuwa na matatizo ya ugumba lakini bado alikuwa na upendo na watoto wa ndugu zake ambao aliwachukua na kuwasomesha hadi sasa mmoja wa watoto hao anasoma Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

 Amesema katika maisha yake ya mateso, aliishi na mwanaume kwa miaka 20 lakini mateso na manyanyaso aliyoyapata ni makubwa na aliamua kumwachia Mungu  mwenyezi.

Wengine waliowaliza viongozi hao ni pamoja na Greciana Pius Kayega, ambapo alisema  katika maisha yake ya ndoa na mume wake ilipokuja kubainika kuwa ni mgumba alipata manyanyaso makubwa kutoka kwa mawifi zake hali ambayo alijitahidi kuivumilia lakini alishindwa.

Naye Makamu Mwenyekiti  Aziza Athumani, Angela Ngoroma na Flora Ulanga wao walijikuta wakitoa machozi tu pasipokusema chochote.

   Mwisho.


 

Previous articleHALMASHAURI YA MALINYI KUWAKAMATA WAVAMIZI BONDE LA MAJI LA MWALIMU NYERERE.
Next articleMAGAZETI YA LEO J.NNE MEI 11-2021

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here