Home BUSINESS WAFUGAJI IGUNGA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MRADI

WAFUGAJI IGUNGA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA YA MRADI


Na: Lucas Raphael Tabora.

WAFUGAJI wilayani Igunga Mkoani Tabora wametakiwa kuchangamkia fursa ya ujio wa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima-Uganda hadi Chongoleani Tanga kupitia wilaya hiyo kama eneo la kuuzia kitoweo cha nyama.   

Ushauri huo ulitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo Igunga, Joseph Sambo alipokuwa akiongea na gazeti hili Ofisini kwake ambapo alieleza kuwa wafugaji wana nafasi kubwa sana ya kunufaika na mradi huo.

Alisema mradi huo ambao upo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji utapita katika ardhi ya wilaya hiyo na kujengwa moja ya vituo vya kusafishia mafuta katika eneo hilo.

Alibainisha kuwa wakati wa ujenzi wa bomba hilo mafundi watahitaji huduma mbalimbali ikiwemo chakula, vinywaji, kitoweo cha nyama, mayai na malazi hivyo akawataka wafuga kuku, mbuzi, ng’ombe na bata kukaa mkao wa kula.

‘Wafugaji wetu jiandaeni kutoa huduma ya kitoweo kwa mafundi na wafanyakazi wa mradi, msiwaachie wauza kuku, mbuzi, bata na ng’ombe kutoa wilaya nyingine waje kutoa huduma hizo’, alisema.

Mkurugenzi Sambo alibainisha kuwa ujio wa mradi huu ni fursa muhimu sana kwa uchumi wa wakazi wa wilaya hiyo, hivyo kila mmoja anapaswa kujiandaa ili mradi utakapoanza, huduma zote zipatikane na wajiongezee kipato.

Aidha alitoa wito kwa wafanyabishara, akinamama wauza chakula (mama ntilie) na watoa huduma za usafiri kujipanga vizuri ili mradi utakapoanza huduma zozote zitakazohitajika zipatikane.

Mtaalamu wa Mifugo wa Mamlaka hiyo Andreas Kafuru alisema kuwa wilaya hiyo na hasa Mji wa Igunga umejaliwa kuwa na mifugo mingi ambayo ni chanzo kizuri sana cha mapato ya wananchi, halmashauri na taifa kwa ujumla.

Alifafanua kuwa mradi huo ni fursa muhimu sana inayoweza kunufaisha sekta ya mifugo na uvuvi kutokana na idadi kubwa ya mifugo iliyopo, alitaja idadi hiyo kuwa ni ng’ombe 687,911 mbuzi 378,951kondoo 213,755 kuku 1,500,253 na nguruwe 62,528.

Aidha aliongeza kuwa idara yake imeendelea kuhamasisha ufugaji wa kisasa ikiwemo kuimarisha na kuboresha miundombinu mfano machinjio, masoko ya mifugo na samaki na mabucha ili kuhakikisha wafugaji wananufaika zaidi.

Mwisho.

Previous articleNCHI WANACHAMA SADC KUANZISHA KITUO CHA HUDUMA ZA KIBINADAMU.
Next articleWATU 23 WAKATWA MAPANGA CHANIKA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here