Na: Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa Mabingwa wa Soka Afrika Mashariki na Kati kwa Wanawake ‘Simba Queens’ Charles Lukula, amesema kuwa kikosi kipo tayari kupambana katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi cha Simba Queens kitaanza Kampeni ya kusaka taji la Afrika Oktoba 30 kwa kucheza na wenyeji AS FAR (Morocco), kwenye Uwanja wa Moulay Hassan, mjini Rabat.
Akizungumza jana katika Mkutano na Waandishi wa Habari Kocha huyo,amesema amefanikiwa kuandaa kikosi chake katika kuelekea kwenye Michuano hiyo.
Ameongeza kuwa amefanikiwa kucheza michezo kadhaa ya kirafikia ambayo imempa kipimo tosha katika michuano hiyo ambayo ni muhimu katika kikosi.
“Kikosi change kipo imara na mpaka sasa hatuna mchezaji ambaye ni majeruhi tunaenda Morocco tukiwa na kikosi kamili,pia tumecheza mechi za kirafiki na timu ipo kwenye hali nzuri ya ushindani.” amesema
Kwa upande wake Nahodha Opa Clement, amesema wachezaji wanajua malengo ni kuhakikisha tunafika nusu fainali ya michuano hiyo japo haitakuwa rahisi.
“Tunawashukuru viongozi wetu kwa sapoti kubwa wanayotupatia, wamekuwa wakiweka mazingira yetu ya kazi kuwa rahisi, kikubwa tunawaomba mashabiki waendelee kutuombea ingawa hawatakuwepo uwanjani,” amesema Opa.
Katika Michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa Wanawake Simba Queens imepangwa ‘Kundi A’ na wenyeji AS FAR (Morocco), Green Buffaloes (Zambia) na Determine Girls (Liberia).
Pia kikosi cha Simba Queens itaanza Kampeni ya kusaka taji la Afrika Oktoba 30 kwa kucheza na wenyeji AS FAR (Morocco), kwenye Uwanja wa Moulay Hassan, mjini Rabat.
Mabingwa Watetezi Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) wamepangwa ‘Kundi B’ sambasamba na timu za Bayelsa Queens (Nigeria), Wadi Degla (Misri) na TP Mazembe (DR Congo).