Home LOCAL MHE. SILAA ATOA MATUMAINI YA KUPATA MAJI KWA WAKAZI WA MGEULE

MHE. SILAA ATOA MATUMAINI YA KUPATA MAJI KWA WAKAZI WA MGEULE

Na: Crispin Gerald

Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Silaa amewapa matumaini wakazi wa maeneo ya Mgeule kuhusu upatikanaji wa maji kwani DAWASA inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusogeza huduma ya maji kwa wananchi walio nje ya mtandao.

Mhe. Silaa ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kutembelea hali ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Mgeule ambao hawapati maji kwa sasa na kuwapa mwelekeo wa lini maji yatapatikana.

Amewataka wananchi kuwa wapole kwa kuwa DAWASA inaendelea kutekeleza miradi mikubwa kwenye maeneo yao ukiwemo mradi mkubwa wa Kibamba – Kisarawe ambao unatoa huduma kwa wananchi wa Pugu, Gongo la Mboto hadi maeneo ya nyeburu.

Pia mradi mwingine ni mradi wa maji nje ya mtandao unaotekelezwa na DAWASA kwa kushirikiana na Benki ya Dunia (WB) kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi walio nje ya mtandao, mradi utanufaisha wakazi 4,444 wa mitaa ya Mgeule na Mgeule juu na kumaliza shida ya maji kabisa.

Kwa ufupi mradi wa maji nje ya mtandao unaotekelezwa unalenga kutoa huduma kwenye maeneo ya Nzasa somelo, Mgeule Juu na Mgeule, yangeyange, na kwenye kata ya Msongola.

Mbali na hayo, ofisi ya DAWASA Kisarawe hutekeleza miradi mbalimbali ya ndani kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya majisafi, hivyo jitihada zote hizi zinazofanywa zinaleta matumaini ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wote.

Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Kihuduma DAWASA Kisarawe Alex Ng’wandu amesema kuwa DAWASA imejipanga kikamilifu katika kutoa huduma ya maji kwa wananchi wote wa maeneo haya kwa kuwa ni haki yao.

Miradi hii inayotekelezwa inalenga kuwezesha upatikanaji wa maji kwa kiasi kikubwa kwa wakazi wote, hivyo tuwatake wananchi wote kuwa na amani wakati utekelezaji ukiendelea na kwamba ndani ya mwaka huu wakazi watapata huduma.

Msimamizi wa mradi wa Benki ya Dunia (WB) Mhandisi Zakaria Kalimbi amesema kuwa mradi wa maji nje ya mtandao unaotekelezwa unalenga kufikisha huduma kwa wakazi 4,444 wa mitaa ya Mgeule na Mgeule juu, Kata ya Buyuni wilaya ya Ilala ambao hawana huduma kwa muda mrefu.

Ameeleza pia kuwa mradi unahusisha ujenzi wa mtandao wa kusambaza maji wa kilomita 23 ambao mpaka sasa wamelaza bomba za inchi 2.5 mpaka 8 kwa umbali wa kilomita 20.

“Huu ni mradi unaotekelezwa kwenye mitaa ya 14 kwa gharama ya bilioni 10.7, kwa mitaa ya Mgeule na Mgeule juu iliyopo kwenye kata ya Buyuni ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huu,” amesema.

Mradi unachukua maji kutoka kwenye chanzo cha mtambo wa Ruvu Juu na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Nae mkazi wa mgeule Bi Shamimu Richard ameeleza kufurahishwa na jitihada zinazotekelezwa na DAWASA za kufikisha huduma kwa wakazi wote.

“Huduma ya maji kwetu ni ya shida sana, lakini kazi hii inayoendelea inatupa matumaini ya kupata huduma hivi karibuni,” amesema.

Previous articleMAGAZETI YA LEO JUMANNE OKTOBA 25 -2022
Next articleWANANCHI SONGWE WATAKIWA KUHESHIMU MAENEO YA HIFADHI YATAKAYOBAKI BAADA YA KUMEGEWA SEHEMU YA HIFADHI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here