EWURA Kanda ya Kaskazini Tar. 20/10/2022 imetoa mafunzo kwa wanafunzi wa kada ya umeme katika chuo cha Ufundi Arusha (ATC), kuhusu utaratibu wa uombaji wa leseni za ufungaji wa mifumo ya umeme.
Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Mha. Lorivii Long’idu, ameeleza kuwa, elimu hiyo itawasaidia wanafunzi hao, kuelewa miongozo mbalimbali ikiwamo sheria na kanuni katika kazi za umeme.
“Elimu hii imelenga kuwaandaa wanafunzi hawa pindi wanapomaliza masomo yao, kuomba leseni ya ufundi umeme EWURA, ili wakafanye kazi kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha sheria ya umeme, inayotaka mtu yeyote kuwa na leseni kutoka EWURA, ndipo afanye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme”
Katika semina hiyo, EWURA imeeleza mahitaji muhimu wakati wa maombi ya leseni za ufungaji wa mifumo ya umeme.
Vilevile uchanganuzi wa madaraja ya leseni za ufundi umeme na masharti ulifafanuliwa kama ilivyoainishwa katika Kanuni za ufungaji wa mifumo ya umeme za mwaka 2022, zinazopatikana katika tovuti ya EWURA www.ewura.go.tz.