Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amebariki mapendekezo ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya kujengwa kwa Hospitali ya Wilaya katika Kijiji cha Chekereni Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro.
Akikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Waziri Bashungwa amesema Kamati ya Fedha , Uongozi na Mipango ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tarehe 19 Agosti, 2021 walifanya maazimio kuwa hospitali ya wilaya ijengwe Kata ya Mabogini.
Waziri Bashungwa ameendelea kufafanua kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya hivyo kamati hiyo ipo sahihi kulingana na miongozo iliyowekwa na Serikali.
Amesema,Serikali ya Awamu ya Sita iliahidi kupeleka maendeleo nchi nzima bila ubaguzi kwa kuwa wananchi wote wanahitaji kupata huduma bora za afya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anakamilisha mchakato wa kijiji kukabidhi ardhi na katika eneo hilo na kijengwe kituo cha afya katika Kata ya Kilua Vyunjo Kusini ili wananchi waweze kupata huduma za afya kwa karibu.
Waziri Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Mhandisi Daniel Kileo kuhakikisha anaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mara moja katika Kata ya Mabogini na kumuagiza Meneja wa TARURA Mkoa kuhakikisha wanajenga barabara katika eneo linalojengwa hospitali hiyo.
Aidha, mgogoro wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya umedumu kwa takribani miezi tisa ambapo tayari kiasi cha shilingi milioni 500 zilishatengwa kwa ajili ya ujenzi huo katika bajeti ya mwaka 2021/2022.