Na: Stella Kessy
KIKOSI cha Simba kimewasili salama Angola kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya de Agosto unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 9, Uwanja wa Novemba 11 uliopo Angola.
Hata hivyo miongoni mwa wachezaji ambao wapo kwenye msafara huo ni kipa namba moja Aishi Manula, Beno Kakolanya na Ally Salim ambao wote hawa ni walinda milango.
Pia washambuliaji ni watatu ambao ni Habib Kyombo, John Bocco ambaye pia ni nahodha pamoja na Moses Phiri. Miongoni mwa mabeki ambao wapo kwenye msafara huo ni Mohamed Hussein na Joash Onyango.
Akizungumza kabla ya kuondoka Kocha Mkuu Juma Mgunda amesema wanatambua wapinzani wao uimara wao ulipo na udhaifu wao ulipo hivyo watapambana kupata matokeo.
“Tunatambua uimara wa wapinzani wetu ulipo na madhaifu yao yalipo, tutatumia madhaifu yao kupata matokeo kwenye mchezo wetu ambao tunajua kwamba utakuwa mgumu,”.