Na: Mwandishi wetu, Mtwara.
MKUU wa mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abasi amewapa ubalozi wa kuutangaza mkoa wa Mtwara mabondia Twaha Kiduku na Karim Mandonga kuelekea kwenye pambano la kimataifa la Mtwara Ubabe Ubabe 2 linalotarajia kupigwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani hapa.
Mabondia hao wamepewa ubalozi huo baada ya kufanya ziara maalum katika bandari ya Mtwara pamoja na Uwanja wa Ngede wa Mtwara wakiwa na mkuu wa mkoa huyo aliyeambatana na mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya kabla keshokutwa kwa mabondia hao kupanda ulingoni kwenye pambano hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Kanali Abasi alisema kuwa wamepewa ubalozi huo mabondia hao katika kuufungua mkoa wa Mtwara kwa kuhakikisha wanautangaza kuvutia wawekezaji kutokana na maendeleo ya bandari na uwanja wa ndege wa kisasa unaelekea kukamilika kutokana na juhudi za serikali katika kuboresha miundombinu ya kiuchumi katika mkoa huo.
“Tumewapa ubalozi ndugu zetu mabondia kuweza kuutangaza mkoani wetu, tumefanya ziara kwenye bandari na pamoja na uwanja wa ndege na wameweza kuona namna sererikali inavyohakikisha tunaufungua mkoa wa Mtwara katika suala zima la uwekezaji na mambo ya utalii kwa watalii kuweza kufika kwa wingi.
“Lakini kubwa niendelee kumshukuru rais kwa uwekezaji huu ambao unaweza kwenda kuufungua mkoa wetu kwa maana ya kuhudumia mkoa pamoja na nchi za jirani, lengine uwanja huu unaenda kufungua za kibiashara katika usafirishaji na mizigo, nimewalata mabondia hawa kama sehemu ya mabalozi kwa mkoa wa Mtwara katika kuutangaza mkoa, “ alisema Kanali Abasi.
Kwa upande wa mabondia hao wameshukuru lakini wamepongeza juhudi za serikali ya mkoa wa Mtwara katika kuhakikisha inasimamia miradi yote ya serikali inafanikiwa kwa kuleta maendeleo huku wakiahidi kuwa mabolozi wakubwa kwa kuweza kuutangaza mkoa huo.