Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya yaIkungi, Gurisha Msemo akitoa maelezo kwa mgeni rasmi wakati wa ukaguzi wa ghala hilo.
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki akisisitiza jambo wakati wa ukaguzi wa mradi huo.
Wauzaji wa pembejeo za kilimo wakiwa kwenye banda lao wakimsubiri mgeni rasmi kutembelea banda lao.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto akiongoza shughuli mbalimbali za uzinduzi huo.
Mtaalamu wa Kitengo cha kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Mwadanga, akizungumzia mradi huo kwa ujumla wake.
Mkurugenzi wa Shirika la Farm Africa, Mary Batterman akizungumzia umuhimu wa ghala hilo kwa jamii.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Koica Tanzania, Kyucheol Eo akitoa taarifa kuhusu mradi huo na umuhimu wake kwa wakulima.
Mwenyekiti Msaidizi wa Kampeni ya Kukomesha Vitendo na Matukio ya Ukatili Dhidi ya Jinsia, Wanawake, Watoto na Wazee iitwayo Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Singida, Ambwene Kajula akiitambulisha kampeni hiyo ambayo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Haika Masawe akitoa taarifa ya ujenzi wa ghala hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la KIWOHEDE, Justa Mwaituka akichangia jambo kwenye hafla hiyo
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga akizungumza kwenye hafla hiyo.
Hati hizo zikikabidhiwa.
Hati ikikabidhiwa.
Zawadi ya mbuzi ikitolewa kwa mgeni rasmi
Na: Dotto Mwaibale, Singida.
MKUU wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge amewataka wakulima kubadilika na kujipanga na kufanya kilimo biashara na kuachana na kilimo cha mazoea.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Mulagiri kwa niaba ya Dk. Dk. Mahenge wakati akizindua ghala la kuhifadhi zao la alizeti lililojengwa na Shirika la Farm Africa katika Kijiji cha Mnang’ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake na Jinsia la Umoja wa Mataifa (UN-WOMEN) kwa gharama ya Sh. 248,324,122 chini ya Ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Korea Kusini (KOICA)
Mulagiri alitaja baadhi ya mambo ya kufanya kilimo biashara ni kuwa na mipango biashara na uzalishaji wa kimkakati, kufahamu kwanza taarifa sahihi za masoko ya alizeti, mahitaji ya soko, wanunuzi, ubora wa mazao, mifumo yao na motisha endelevu za kufanya biashara na wakulima.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kutumia teknolojia zana bora, mbegu bora na pembejeo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, wakulima wajiunge kwenye Ushirika/ vikundi na kuuza kwa pamoja ili kuwa na bei yenye tija, watumie fursa ya kuzungumza na wanunuzi kabla ya kuanza kuzalisha mfano kilimo cha mkataba.idha Mulagiri alisema wafanyabiashara wakubali kuwekeza katika uzalishaji kupitia kilimo cha mkataba baina ya Ushirika/ vikundi vya wakulima na wanunuzi na kuwa zao la Alizeti lina fursa kubwa ya wakulima kupata soko na kujipatia kipato hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa mahitaji ya soko ni zaidi ya mara 3 ya kiasi kinacho zalishwa kwa mwaka.
Mulagiri alitumia nafasi hiyo kuagiza kutumia ghala hilo ambalo pia litatumika kama Kituo cha Huduma za Wakulima kwa kutafakari, na kila mdau kujipanga na Kukuza uelewa wa pamoja kati ya wadau kuhusu mnyororo wa thamani wa zao la alizeti,hususani majukumu kati ya kuzalisha na kuuza kwa tija ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na uratibishaji bora miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani wa zao la alizeti.
Alisema wakulima wadogo kupitia ushirika na vikundi vyao waunganishwe na masoko makini na yenye tija akitolea mfano Kilimo cha Mkataba na kuachana na mambo ya kuomba omba na kueleza kuwa wanunuzi au taasisi za fedha wawezeshe wakulima kupata pembejeo na fedha za kilimo kupitia mikopo rafiki yenye masharti na riba nafuu inayoendana na hali ya wakulima na kilimo chao kwa ujumla.
“Wakulima wajipange kulima kibiashara na kuhakikisha kuwa wanayajua vema mahitaji yao, wapi pa kuyapata na kwa muda gani na kujenga uelewa wao juu ya vichochei na fursa za kilimo endelevu endelevu. Sio leo msimu mmoja tu umekopeshwa kulima hulimi, kulipa hutaki na unaposhindwa kutimiza Wajibu wako huji hutoi ushirikiano, hiyo haikubaliki kabisa ni lazima tufikiri kilimo kama biashara nyingine” alisema Mulagiri.
Mulagiri aliongeza kuwa wataalam wa kilimo waendelee kuchukua jukumu la Kujenga uwezo wa wadau muhimu katika uwajibikaji wa pamoja katika uzalishaji, usimamizi wa uzalishaji, ukusanyaji wa mazao, mchakato wa kuuza kwa pamoja, kusimamia ubora na mikakati endelevu ya kukuza biashara ya Alizeti.
Aliwataka wataalam hao wapate uzoefu na tathmini ya mafanikio na changamoto za mnyororo wa thamani wa zao la Alizeti, kuendeleza mikakati husika kwa ajili ya ufanisi wa biashara ya Alizeti, kuimarisha ushirikiano na kuwajibika miongoni mwa wadau na kuwa na mijadala huru ya kibiashara na vishawishi muhimu vya biashara ya Alizeti na kutambua maeneo muhimu ya kuboresha utekelezaji na ufuatiliaji wa maendeleo ya uzalishaji na Uuzaji wa ya Alizeti.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza kwenye uzinduzi huo alisema kupata ghala ni kitu kimoja na kulitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ni jambo jingine akieleza kuwa kuna mifano inajionyesha kwani yapo maeneo mengi hapa nchini yamejengwa maghala lakini sasa yamekuwa ni kumbi za mikutano na disko na ndio maana kwa Ikungi wamejiongeza kwa kutafuta mfumo uliobora wa matumizi ya ghala hilo liweze kuwa na tija.
Muro aliomba zitengenezwe kanuni au sheria ndogo zitakazotumika kuliendesha ghala hilo na kuwa wakati kipindi hiki ambacho Taifa linapambana na nakisi ya zaidi ya tani 500,000 ya mafuta ya chakula kuagiza nje ya nchi kwa Mkoa wa Singida ni fursa ya kuashiria alizeti sasa ni Tanzanite na dhahabu na ni zao lenye thamani kama yalivyo mazao mengine makubwa kama pamba, korosho na kahawa.
Aliwataka wakulima kutulia na kuacha kufanya kilimo cha mazoea badala yake walime kilimo chenye tija huku akitolea mfano wakati wakipata Sh.300,000 kwa kilimo kisicho na tija wenzao wanapata zaidi ya Sh.Milioni 1 kwa kilimo chenye tija hivyo hatakubali kuona wakulima wakinyonywa na vishoka kwa kununua gunia la alizeti kwa Sh.30,000 na wao kuliuza kwa Sh.70,000 wakati hawalimi, hawana mashamb wala hawanunui mbegu labda awe hayupo katika wlaya hiyo.
“Mwaka huu nimekubali kujitoa kafara ili kumbadilisha mkulima na usipokubali kubadilika nitakubadilisha kwa nguvu na utabadilika, tumechoka kila mwaka tunalima pesa haitoshi nataka wakulima wangu wa wilaya ya Ikungi tulime mjenge nyumba za kisasa, tupate magari na watoto wetu wapate mitaji na si tulime kwa ajili ya chakula nitazameni tu nimeletwa hapa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuyabadilisha maisha yenu na si vinginevyo” alisema Muro.
Alisema wataanzisha mfumo wa kuyachukua alizeti kwa wakulima hao kwa hiyari na hata kwa kutumia nguvu na kwenda kuitunza kwenye ghala hilo baada ya kufanyika kwa utaratibu maalum wa kuzipokea lengo likiwa ni kumsaidia mkulima.
Alisema Serikali wilayani humo imejipanga kumsaidia mkulima ambaye atakuwa na subira ili alizeti anayoilima iwe msaada wa kubadili maisha yake ambapo alitumia kuwaomba wakina mama kuwahimiza waume zao kupeleka alizeti kuhifadhiwa katika ghala na kuja kuiuza kati ya Sh.80,000 hadi 100,000 badala ya Sh.30,000 na Sh.40,000.
Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkazi wa UN-WOMEN Tanzania, Mratibu wa Mradi wa Tuufikie Usawa wa Jinsia kupitia kuwawezesha Wanawake na Wasichana, Lilian Mwamdanga alisema mradi huo unatekelezwa na UN-WOMEN kwa kushirikiana na UNFPA kupitia ufadhili wa Koica na kuwa UN- Women imekuwa ikiongoza kipengele cha kuwezesha wanawake kiuchumi hususan kuwajengea uwezo wanawake wakulima wadogowadogo katika mazao ya mboga mboga na alizeti katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kuwa uzinduzi wa ghala hilo ni sehemu ya mradi huo.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili mradi huo umewafikia wakulima zaidi ya 1000 ambao ni wa mboga mboga na alizeti kutoka katika Kata za Sepuka, Irisya na Dung’unyi na kati yao wanawake ni asilimia 80.
Akitoa taarifa ya utekeleza wa mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Afisa Maendeleo ya Jamii wa wilaya hiyo, Haika Masawe alisema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya zao la alizeti kwa kutunza mazao yao kwa pamoja wakisubiri bei yenye tija ili kuwawesha wanachama/wakulima kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.
Masawe alisema ujenzi wa ghala hilo ulianza Mwezi Novemba mwaka 2021 na kukamilika mwezi wa Machi mwaka 2022 chini ya mkandarasi Manyara Contractors akisimamiwa na Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na Mkuu wa Idara ya Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika.