BUKOBA:
KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi an Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, CPA Amos Makalla amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mkombozi kwa kuinua zao la Kahawa mkoani Kagera.
Makalla ameeleza hayo leo Mei 18,2025 akizungumza na wananchi katika Wilaya ya Bukoba Mjini mkoani Kagera akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku saba katika mikoa ya Kanda ya ziwa.
Makalla ameeleza kuwa wananchi ni mashahidi namna watu walivyokuwa wakihangaika na uuzaji wa zao hili katika mkoa huo na kwa busara za Rais Samia akasaidia kuinua kwa kuongeza bei ya zao hilo kutoka elfu hadi 6,500.
“Nyie mnajua historia ya kahawa katika mkoa huu watu wamehangaika, magendo ya Kahawa kwenda Uganda manakumbuka msako ulivyokuwa watu wanahangaikia kuuza kahawa amekuja rais, mama yetu kwa busara zake na uzalendo wake ametutoa kwenye bei ya 1000 mpama 6000 hadi 6,500,” amesema Makalla.
Makalla amewataka wananchi kuacha kuhadaika na maneno ya uongo yanayopelekwa na watu kwa lengo la kufanya uchochezi kwa kusema serikali haijafanya kitu chochote, huku wakiwa hawajua undani wa jambo hilo.
Ameongeza sio kahawa tu bali ni katika zao la Kokoa, Ufuta, mbaazi ambayo yameongezeka thamani ya mauzo yake kwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.