WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali ipo kazini na inaendelea kufanyakazi ya kuwahudumia na kuwatumikia wananchi katika maeneo yote nchini na bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi waendelea kushirikiana katika kudumisha amani na utulivu na kwamba wasiwasikilize watu wenye viashiria vya uvunjifu wa amani wanaopita katika maeneo yao.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Mei 18, 2025) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kwideko, Kata ya Ngudu wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
”Huu ni wakati ambao watumishi wote wanatakiwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao na kuwaeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya maendeleo yao, ambapo alitolea mfano mradi wa VETA unaojengwa katika wilaya ya Kwimba kwa gharama ya takribani shilingi bilioni mbili.”
Waziri Mkuu amesema wakazi wa wilaya hiyo wanatakiwa kuchangamkia fursa ya ujenzi wa mradi huo kwa kwenda kusoma na kupata ujuzi wa fani mbalimbali ambazo zitawawezesha kujiajiri au kuajiriwa hivyo kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kuhusu upatikanaji wa mitaji, Waziri Mkuu amewasihi wananchi hao kuwasilisha mawazo yao ya biashara katika taasisi mbalimbalib za kifedha ambazo zinatoa mikopo.
Pia, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kwimba Dkt. Amon Mkonga na Maafisa elimu wafanye mapitio ya ikama ya walimu katika shule za wilaya hiyo na kuhamisha walimu kutoka kwenye shule zenye walimu wengi na kuwapeleka katika shule zenye walimu wachache ili nazo ziwe na walimu wa kutosha.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na maelekezo na maagizo anayoyatoa kwa Wizara hiyo ya kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika maeneo yao.
Awali, Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na amemtaka mkandarasi ahakikishe anakamilisha mradi huo kwa wakati.
Ujenzi wa jengo hilo la utawala unaotekelezwa katika kata ya Ngudu Wilaya ya Kwimba ulianza tarehe 27/12/2021 ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi bilioni 3.45. Mradi huo ambao upo katika hatua za ukamilishwaji utawawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.