Home BUSINESS KKKT KUSHIRIKIANA NA TRA KUTOA ELIMU YA KODI

KKKT KUSHIRIKIANA NA TRA KUTOA ELIMU YA KODI

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) linatarajia kuanza kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoa elimu ya Kodi makanisani ili kuongeza idadi ya walipakodi Kodi kwa hiari na kuleta usawa katika ulipaji wa Kodi.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja baina ya Askofu Mkuu wa KKKT Dk. Alex Malasusa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda tarehe 30.01.2025, pindi Kamishna Mkuu Mwenda alipomtembelea Askofu Malasusa kwa lengo la kumshukuru kwa kushirikiana na TRA na kuomba ushirikiano zaidi wa kutoa Elimu kwa Mlipakodi.

Thank you for reading this post, don't forget to subscribe!

Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika Azania Front Dar es Salaam, Askofu Mkuu Dk. Malasusa ameahidi kuwa KKKT itashirikiana na TRA kutoa elimu ya Mlipakodi makanisani ili kuongeza idadi ya walipakodi maana Kodi ndiyo damu ya Tanzania.

“Kama ilivyo kwa binadamu hawezi kuishi bila damu mwilini ndiyo ilivyo kwa nchi haiwezi kwenda bila Kodi hivyo kila mmoja wetu anapaswa kutimiza wajibu wake katika kulipa Kodi maana hata Vitabu vya dini vinatutaka kutii Mamlaka” Dk. Malasusa.

Dk. Malasusa amesema Kanisa linatamani kuona nchi inapiga hatua kimaendeleo hivyo ili matamanio hayo yafikiwe ipo haja ya kushiri kikamilifu kutoa elimu ya Kodi ili kila mmoja atambue umuhimu wa kulipa Kodi na kutekeleza wajibu wake.

Amesema katika siku za karibuni wameshuhudia hamasa kubwa ya uhiari katika kulipa Kodi jambo ambalo limeileta Jamii karibu na TRA kupitia ziara za viongozi wa Mamlaka hiyo kwa walipakodi akiwemo Kamishna Mkuu Mwenda.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema TRA imejipanga kushirikiana na viongozi wa Dini mbalimbali nchini katika kutoa Elimu kwa Mlipakodi ili kuongeza wigo wa kodi na kuleta usawa.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema usawa katika Kodi pia utaletwa kwa kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa njia mbalimbali ikiwemo kutokutoa risiti za mauzo na kutumia stempu bandia kwenye bidhaa za vileo.

Amesema kwa kushirikiana na wadau mbalimbali TRA ipo macho ili kuhakikisha hakuna ukwepaji Kodi unaofanyika nchini kwa kuziba mianya yote ya ukwepaji Kodi huo ikiwemo uingizaji wa mali na bidhaa za magendo.

Tangu ateuliwe kuiongoza Taasisi ya TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda amekuwa na utaratibu wa kuwafuata walipakodi na kuwashukuru kwa kuendelea kulipa Kodi huku akiomba ushirikiano zaidi wa kulipa Kodi kwa hiari jambo ambalo limekuwa na manufaa kwa kusaidia TRA kuongeza makusanyo.