Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji (wa kwanza kushoto mwenye nguo nyekundu) akiwasili katika kiwanda cha kuchakata Mkonge cha 21st Century Textiles Limited alipofanya ziara kwenye kiwanda hicho leo Juni 17,2022 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt Ashatu Kijaji akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata mkonge cha 21st Century Holdings LTD leo Juni 17,2022 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali imejipanga kuchukua hatua madhubuti za kutatua changamoto zote zinazoikabili sekta ya viwanda nchini hususani vile vinavyochakata na kuzalisha bidhaa za katani ili viweze kufanya shughuli zake katika mifumo sahihi iliyowekwa na serikali.
Kauli hiyo ameitoa leo Juni 17,2022 Jijini Dar es Salaam alipozungumza 21st Century Holdings LTD kinachojihusisha na uchakataji wa kamba zinazotokana na mkonge kilichopo chang’ombe kilichopo Jijini humo.
Akiongea na wafanyakazi hao Dkt. Kijaji amesema katika kutatua changamoto hizo Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mazao yote yanayotokana na zao Mkonge ikiwa ni lalamiko lao kubwa la wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa za katani.
Pia Amesema Serikali inaendelea kushughulikia changamoto nyingine ili kuviwezesha viwanda hivyo kushiriki kikamilifu katika soko la ushindani ndani ya nchi, kikanda na kimataifa.
Aidha, Dkt. Kijaji amewahakikishia wafanyakazi wa kiwanda hicho kuwa kiwanda hicho hakitafungwa kwa kuwa Serikali inashughulikia changamoto zinazokikabili kiwanda hicho pamoja na zinazowakabili wafanyakazi hao ikiwemo upatikanaji wa maslahi na haki zao za msingi.
Amesema katika kuhakikisha viwanda hivyo vinakuwa na mazingira wezeshi imeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mazao ya Mkonge ambalo ndio malighafi kuu katika viwanda hivyo.
“Katika Mwaka wa fedha ujao Serikali inatarajia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Viwanda ili kila muhusika wa eneo hilo anufaike hatimaye kuongeza ajira na uchumi kwa ujumla hapa nchini”. Amesema Dkt. Kijaji.