Na: Farida Mangube,MOROGORO.
Serikali imeshauriwa kuongeza kasi katika tafiti na upimaji wa maeneo yenye Madini ili kuwasaidia wachimbaji wadogo,ambao kwa sasa wanafanya shughuli hiyo kwa kubahatisha hali inayotajwa kuchochea migogoro na uharibifu wa mazingira kwenye maeneo yanayosadikiwa kuwa na madini.
Hayo yameelezwa na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Vito maarufa kama Spinel katika migodi ya Epanko Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kwenye ziara ya waandishi wa habari yenye lengo la kujifunza na kujionea kazi zinazofanywa na wachimbaji wa madini ili waweze kuwa na uelewa mapana katika kuandika habari za wachimbaji hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika katika migodi hiyo wachimbaji hao waliiomba Serikali kufanya tafiti na kuainisha maeneo yenye madini ili waondokane na tabia ya kuchimba kwa kubahatisha.
Jacob Manyangu ni mmoja wa wachimbaji wadogo katika migodi Epanko alisema licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo miundombinu mibovu ya barabara inayokwenda kwenye migodi hiyo hali inayosababisha kutofikika kwa urahsi pamoja na kuharibu vyombo vyao vya usalifiri, ambapo ameiomba serikali kuwajengea barabara hiyo.
Aidha walisema kama serikali itaweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo ikiwemo utoaji leseni usio na mlolongo mrefu hali inayowafanya wakate tamaa na kujiona hawana thamani ukilinganisha na wachimbaji wakumbwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ruby International LTD ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe. Salim Hasham alisema katika migodi hiyo kuna zaidi ya wachibaji wadogo 300 wanaojishughulisha na uchimbaji na kulifanya Jimbo hilo uchumi wake ukue kwa kasi zaidi kutokana na mzunguuko wa fedha.
Mhe. Salim aliiomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuweka kipaombele katika utambuzi wa madini kitaalam pamoja na kuainisha maeneo yanayofaa kwa uchimbaji,ambapo alisema hali hiyo itawasaidia wachimbaji wadogo kuacha kuharibu mazingira.
Aidha alisema bado kuna changamoto ya wataalam wa madini ya Vito hapa nchini kwani wengi waliopo wamebobea katika aina nyingine za madini hali inayofanya migodi hiyo kukosa wataalam wa kutosha na kufanya shughuli ya uchimbaji kwa mazoea.
Kutokana na changamoto hiyo Mhe. Salim ameiomba serikali kupitia vyuo vya madini hapa nchini kuwapeleka wanafunzi wakajifunzi katika migodi hiyo hali itakayosaidia kuzalisha wataalam wengi zaidi wenye ujuzi wa madini ya vito.
Aidha alisema katika migodi hiyo kuna changamoto ya mawasiliano ya simu pamoja na nishati ya umeme hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji kwani kwa sasa wanatumia jeneleta katika kusukuma mitambo mbalimbali katika migodi hiyo.
Tangu mwaka 2015 uchimbaji katika eneo hilo la Epanko hufanyika chini ya mwekezaji mzawa kampuni ya Ruby International LTD inayomilikiwa na Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe. Salim Hasham .
Kwa mujibu wa Chama cha wachimbaji wa Madini Mkoa wa Morogoro, kuna kiwango kikubwa cha Madini ukilinganisha na maeneo mengine.
Kwa Morogoro pekee zaidi ya shilingi Bilion 2.35 zimekusanywa kwa mwaka 2020-2021, kuna ongezeko la takwimu za Uzalishaji na biashara ya Madini mwaka hadi mwaka.
Asilimia kubwa ya wanaojishughulisha na uchimbaji wa Madini kwa Mkoa wa Morogoro ni wachimbaji wadogo ambapo zaidi ya Leseni 2000 za wachimbaji hao wadogo, Leseni za Uchimbaji wa kati ni 12 pekee na hakuna kabisa wachimbaji wakubwa.
Mwisho.