Mkuu wa wilaya ya Tanga, Mhe. Hashim Mgandilwa amewataka Maafisa Biashara kutumia mafunzo waliyopatiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuwawezesha wafanyabiashara kukua.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo juu ya Sheria ya Leseni za Biashara yaliyofanyika Jijini Taga, Mhe. Mgandilwa amesema, Maafisa Biashara mara nyingi wamekua wakisahau kabisa kazi zao na kuona kuwa wajibu wao mkubwa ni kudai leseni za biashara.
“Maafisa Biashara mara nyingi utawaona kwenye magari wakipita kuzunguka kwenye biashara mbalimbali na kuuliza leseni inamalizika lini na ikiwa itakutwa leseni hiyo muda wake umekwisha wanawadai wafanyabiashara hao bila kuwaelimisha,”amefafanua Mhe. Mgandilwa.
Mhe. Mgandilwa amesema kuwa ni Imani yake kuwa mafunzo waliyopatiwa na BRELA kwa siku tano watakuwa wamewezeshwa jinsi ya kuwajengea uelewa wafanyabiashara kwa kuwapatia elimu kuhusu kukuza biashara zao badala ya kila wakati kwenda kudai leseni za biashara na kwa kufanya hivyo watakuwa wanatekeleza majukumu yao kikamilifu.
Aidha Mhe. Mgandilwa ameipongeza BRELA kwa kufika katika ngazi za chini, kutoa elimu kwani hali hii imeondoa dhana ambayo ilijengeka miaka mingi kwa taasisi nyingi za serikali kujifungia ofisini na kutekeleza majukumu yao wakiwa ofisini tu bila kuwafikia wadau.
Ameongeza kuwa kitendo cha kuamua kutoka na kufika katika ngazi ya chini, kitaongeza uelewa na pia kutengeneza mtandao ambao utapunguza urasimu na malalamiko kwa wananchi.
Mafunzo hayo ya siku tano yalihusisha Maafisa Biashara kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, yalilenga kuwajengea uwezo na uelewa juu ya Sheria ya Leseni za Biashara ambayo imekuwa ikitumiwa na maafisa biashara katika kutekeleza majukumu yao, hasa katika utoaji wa Leseni za biashara kundi ‘B’ ambayo inatolewa katika nagazi ya Halmashauri na Leseni ya biashara kundi ‘A’ ambayo inatolewa na BRELA.
-Mwisho –