️ *_Biashara kufanyika kidijitali kupitia Soko la Bidhaa Tanzania-TMX_*
️ *_Waziri Mavunde kuwa Mgeni Rasmi Hafla ya Mnada_*
️ *Wanawake wahamasishwa kuchangamkia fursa za biashara katika mnyororo wa madini_*
*Mirerani- Manyara*
Wafanyabiashara wa Madini nchini Tanzania wameelezea matumaini yao makubwa kuhusu hatua ya kurejeshwa kwa Minada ya Madini katika eneo Mirerani, Mkoa wa Manyara na kueleza kuwa kurejea kwa minada hiyo kutasaidia kuleta mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya madini, hususan Tanzanite, ambayo ni madini adimu yanayopatikana nchini Tanzania pekee.
Hayo yameelezwa kwa nyakati tofauti na baadhi ya wafanyabiashara wakati wakizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini leo Desemba 13, 2024 kuelekea Siku ya Mnada wa Madini ya Vito Mirerani 2024 inayotarajiwa kufanyika Desemba 14, 2024.
Wafanyabiashara hao wameitaka Serikali kuendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa minada inafanyika mara kwa mara, kwa uwazi, na kwa misingi ya haki, ili kutoa faida kwa pande zote zinazohusika. Kwa pamoja, wanatarajia kuwa kurudi kwa minada ya madini Mirerani kutakuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha thamani ya madini ya Tanzania na kukuza uchumi wa taifa.
Akizungumzia Mnada huo, Mfanyabiashara wa Madini (Dealer) Upendo Kibona ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Lucid Dream Limited amesema kuwa kurejea kwa minada ya madini Mirerani itaongeza uwazi katika soko la madini na kuhakikisha kuwa wauzaji wanapata bei stahiki kutokana na ushindani wa moja kwa moja kati ya wanunuzi.
“Kwa kweli tunaishukuru sana Serikali kwa kurejesha minada hii, kwasababu inatupa fursa ya kuuza madini yetu kwa bei ya ushindani, pamoja na kuwa huu ni mnada wa ndani lakini utasaidia kuongeza ushindani katika bei, na hata hiyo minada ya kimataifa itakapoanza nadhani tutakuwa sehemu nzuri zaidi” amesema Kibona.
Kwa upande wake, Broker wa Madini Glory Robinson amesema, matarajio yake ni kuona minada hiyo inachochea uchumi wa ndani kupitia ajira na biashara ndogo ndogo zinazotegemea shughuli za madini na kwamba Mirerani inaweza kuwa kitovu cha maendeleo ya kiuchumi kwa Mkoa wa Manyara, kwa kuwa minada huvutia wanunuzi wa ndani na nje ya nchi, ambao pia hutumia huduma za hoteli, usafiri, na bidhaa nyingine za ndani.
“Niwahamasishe wanawake wenzangu kuchangamkia hii fursa, kwa sababu kupitia biashara zilizopo kwenye mnyororo mzima wa shughuli za madini zinaweza kuwasaidia kuinua vipato vyao na kuendesha maisha yao sambamba na kutunza Familia zao” amesisitiza Glory.
Naye, Broker wa Madini Sweety Nkya, amesema kuwa Serikali imeonyesha dhamira ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa zaidi kwa pato la taifa ambako kupitia mifumo hiyo ya Minada, biashara itafanyika kwa haki na washindi watapata haki yao ya kimsingi ya kununua na kuuza madini.
“Kurejeshwa kwa minada Mirerani ni ushahidi wa nia ya Serikali ya kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinasimamiwa kwa manufaa ya Watanzania wote, huu mfumo wa minada ni mzuri na elimu iendelee kutolewa kwa wingi ili watu waone manufaa na kujiingiza kwenye hii biashara” amesema Nkya.
Awali, akizungumzia mfumo wa kidijitali unaotumika katika biashara hiyo Afisa Mwandamizi Biashara kutoka Soko la Bidhaa Tanzania (Tanzania Mercantile Exchange-TMX) Nicholaus Kaselwa amesema, Soko la Bidhaa Tanzania ni mfumo rasmi unaokutanisha wauzaji na wanunuzi kwa pamoja na kufanya biashara ya mkataba inayotoa uhakika wa ubora, ujazo na malipo hivyo ili kupata mafanikio makubwa inahitaji uwekezaji wa kisasa wa maghala.
“Sisi tuna mfumo wa biashara ambako soko la bidhaa kama mnada huu hufanyika kwa kutumia mfumo wa kidijitali ambao huwawezesha wanunuzi wa bidhaa kufanya manunuzi popote walipo na kuweka bei zao za ushindani, mwenye bei nzuri hutangazwa mshindi na hupewa masaa 48 kulipia bidhaa na kuja kuchukua” ameongeza Kaselwa.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Hafla ya Mnada wa Madini ya Vito Mirerani 2024 unaotarajiwa kufanyika Jumamosi hii Desemba 14, 2024 Mirerani Mkoani Manyara.
http://KURUDI KWA MINADA YA MADINI MIRERANI KUTASAIDIA KUONGEZA THAMANI YA MADINI – WADAU MADINI