Na WAF, NJOMBE
Wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika halmashauri za mkoa wa Njombe watatatua changamoto za kiafya zinazojitokeza ndani ya jamii ikiwa ni pamoja na udumavu na ukosefu wa lishe bora.
Hayo yamebainishwa Novemba 15, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Bi. Judica Omari alipotembelewa ofisini kwake na timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) na mdau kutoka Taasisi ya Benjamin Mkapa ambao wapo mkoani humo kufuatilia jinsi Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya ngazi ya jamii unavyoendelea, unavyofanya kazi kulingana na matarajio ya Serikali.
Bi. Omari amesema ni dhahiri kuwa mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na changamoto ya udumavu unaoambatana na lishe duni hivyo ni matumaini ya mkoa wa Njombe kuwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakapohitimu mafunzo yao pamoja na mambo mengine watatoa elimu na kuhamasisha wananchi kuzingatia masuala ya lishe bora.
“Nimatumaini ya mkoa wetu kuwa wahudumu hawa wa ngazi ya jamii watatoa huduma bora kwa wananchi baada ya kupatiwa mafunzo na kutakuwa na huduma harakishi kwa kuboresha masuala ya afya ya lishe mkoani Njombe,” amefafanua Bi. Omari.
Awali Mratibu wa Huduma za Afya ngazi ya Jamii kutoka OR-TAMISEMI, Dkt. May Alexander amemueleza Katibu Tawala kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI imeratibu zoezi hilo kwa kuanza na mikoa 10 ambapo wahudumu ngazi ya jamii kwenye mikoa hiyo wanapatiwa mafunzo kwa muda wa miezi sita na kisha kusambazwa katika maeneo yao kwa ajili ya kutoa huduma za afya ya msingi.
“Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa mikoa 10 ambayo imeteuliwa wakati wa awamu ya kwanza kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ngazi jamii na kwa kuanzia wahudumu hao wanaopata mafunzo ni wa kutoka halmashauri ya mji wa Njombe na Makambako,” amefafanua Dkt Elexander.
Mafunzo haya maalumu yanatolewa ndani ya vyuo vya Afya vya Serikali na Binafsi, mkoani Njombe vilivyopo halmashauri ya mji wa Njombe na kimoja kilichopo Halmashauri ya mji wa Makambako ambavyo ni Taasisi ya Afya na Sayansi Shirikishi Njombe, Chuo cha Afya cha Mgao, na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Makambako.
Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango Januari 31 ,2023 huku mikoa 10 iliyo katika awamu ya kwanza ya mpango huu ni Njombe, Mbeya, Songwe, Tabora, Kigoma, Geita, Kagera, Lindi, Mtwara na Pwani.