Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wametakiwa kuvuna uzoefu kutoka kwa Mabalozi Wastaafu na wabobezi ambao waliupata baada ya kutumikia nchi hii kwa uadilifu mkubwa na kusaidia kupaisha diplomasia ya Tanzania ulimwenguni.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Said Shaib Mussa wakati anafungua mafunzo ya Mawasiliano ya Kidiplomasia kwa watumishi wa Wizara yanayofanyika jijini Dodoma kwa siku tano kuanzia tarehe 11 hadi 15 Novemba 2024.
Mhe. Balozi Mussa alisema Wizara imeandaa mafunzo hayo na kuleta Mabalozi wastaafu na wabobevu kuyaendesha ili kuwajengea uwezo watumishi kuwa na ujuzi na mbinu bora za kufanya mawasiliano sahihi kwa kutumia nyenzo za mawasiliano za kidiplomasia zinazotumika duniani kote.
“Tuwe wasikivu na tuzingatie maelezo ya wakufunzi wetu ili tukimaliza mafunzo haya, tuweze kufanya mawasiliano yanayozingatia lugha sahihi na muda sahihi kwa wadau wetu wa ndani na nje ya nchi”, Balozi Mussa alisema.
Amesema kuwa Wizara inakusudia kuwa na mwendelezo wa mafuunzo haya ili kuwawezesha watumishi wake kuwa na mbinu na ujuzi stahiki wa kuchambua masuala ya kimataifa yanayotokea duniani na namna yatakavyosaidia nchi, na kuendana na mabadiliko ya dunia katika nyanja ya kidiplomasia.
Mwakilishi wa Mabalozi hao, Balozi Bertha Semu-Somi alisema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwao katika kipindi chote walichoitumikia, hivyo, wapo tayari wakati wote kutoa uzoefu wao, kwani kufanya hivyo, kwao ni kama kurejesha kwa Serikali.
Aidha, mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Bw. Charles Mbando wakati anatoa neno la shukrani aliiomba Wizara iendelee na utaratibu huo, tena katika fani tofauti tofauti ili watumishi wapate ujuzi sahihi utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo kulingana na mahitaji ya dunia ambayo hubadilika kila wakati.
Mabalozi wengine wanaoendesha mafunzo hayo ambayo ni ya awamu ya tatu, ni Balozi Mohammed Maundi; Balozi Tuvako Manongi; Balozi Peter Kallaghe; Balozi Begum Taj na Bw. Khamisi Abdallah.